Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) imevitaka vyombo vya sheria kuwachukulia hatua Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Sisty Nyahoza na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Awadhi Juma Haji ili wawajibike na wawajibishwe wao kama wao kisheria kwa kusababisha maumivu kwa viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika tukio la hivi karibuni.
Katika tamko lake ililolitoa kwa wanahabari kupitia kwa Mwenyekiti wake Taifa Sospeter Mosewe Bulugu, SMAUJATA imeeleza kujiridhisha na maelezo ya viongozi wakuu wa CHADEMA kupitia mkutano na vyombo vya habari waliouitisha siku moja baada ya kuachiwa huru, na yale ya mashuhuda kuwa Kamishna Awadhi Haji alitumia “nguvu kubwa sana kuwadhalilisha” viongozi wa upinzani bila ushahidi wa msingi wa shutuma dhidi yao.
“Kauli ya Kiongozi wa baraza la Vijana wa CHADEMA BAVICHA, ndugu Mwaipaya Ilikuwa kauli ya kawaida sana kisiasa kwa watu ambao wanakwenda kukutana eneo la wazi na lililotajwa la Ruanda Nzovwe Jijini Mbeya kama vijana, siku inayotambuliwa kidunia na kwamba Jeshi la Polisi lilipaswa kuelekeza nguvu katika kuwalinda vijana”, imeeleza SMAUJATA.
Aidha imeeleza kuwa Awadhi na Nyahoza wanapaswa kuwajibika kwa namna yoyote ili iwe funzo kwa watu wenye nia ovu ya kuzua taharuki na wenye kutumia nafasi zao vibaya ndani ya Ofisi za Serikali na majeshi yaliyopo kisheria kwa kutenda uhalifu, kuvunja sheria na kufanya visasi kwa kile ilichokieleza kuwa masilahi binafsi.
“Kwa maelezo ya viongozi waliotendewa ukatili huu ambao ni wazi kuwa hawakukaidi wito wa polisi na hata baada ya kujisalimisha waliendelea kupigwa, kuteswa gizani kama magaidi, watu ambao hata hivyo hawakuwa na silaha yoyote iliyoashiria kuwa na njama za kutenda makosa ya uvunjifu wa amani”, imeeleza jumuiya hiyo.
Katika hatua nyingine, SMAUJATA imesema kuwa matukio yaliyofanywa na Nyahoza na Awadhi ni njama za makusudi za kumchafua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameelezwa kufanya “jitihada kila siku za kuleta amani na maridhiano” katika taifa kupitia falsafa ya 4Rs.
Aidha SMAUJATA imependekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Polisi, na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kufanya uchunguzi wa haraka, wa kina, na wa huru kuhusu tukio hilo ili kubaini ukweli na kuhakikisha kuwa wahusika wanawajibishwa kisheria.