Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam, wilayani Ilala, Mkoani Dar es salaam Elihuruma Mabelya amemthibitishia Waziri wa ofisi ya Rais, tawala za Mikoa na serikali za mitaa Mohamed Mchengerwa, Ilala itaendelea kuwa kinara wa ukusanyaji mapato kupitia miradi inayobuniwa.
Mabelya ameyasema hayo wilayani Ilala, katika kata ya vingunguti, wakati anaeleza juu ya mradi wa Soko jipya la nyama choma ambalo ni la kwanza ndani ya jiji la Dar es salaam kujengwa kisasa ili liweze kuingizia mapato.
Amesema Soko hilo limegharimu kiasi cha Shilingi Mil.729.6 kukamilika kwake zilizotokana na mapato ya ndani na litachukua zaidi ya wafanyabiashara 232 tofauti wakiwemo wachoma nyama, mama lishe na baba lishe, wauza maduka na vinywaji.
Amebainisha kuzinduliwa kwa soko hilo kunaenda kuchochea ukuaji uchumi kwa makundi ya wafanyabiasha wadogo ambao ndiyo wanufaika wa mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na jiji kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Ameongeza kuwa kupitia ufunguzi wa soko hilo, Ilala itaendelea kubuni miradi mbalimbali yenye lengo la kuongeza mapato ya ndani na miradi inayokuwa karibu na wananchi katika kukuza ushirikiano na kutatua changamoto ya masoko.
Mabelya, amemhakikishia Waziri Mchengerwa kuwa viongozi wa Ilala, wataendelea kuwatumikia wananchi kwa kufanya kazi kwa ushirikiano, viongozi kutumia weledi katika kuhakikisha maendeleo yanaonekana kwa wananchi.
Aidha Mkurugenzi huyo wa Jiji la Dar es salaam, Elihuruma Mabelya amefafanua Halmashauri ya Ilala imevunja mikataba 17 ya miradi ambayo ilikuwa inasusua ambayo ilikuwa haiendani na kasi ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo ya mfano waliyovunja ni mkataba na wakandarasi pamoja na ule wa Kituo cha Afya Mzinga ambao ulikuwa ukamilike 2018, Mradi wa ujenzi Shule ya Sekondari Bonyokwa, Mradi wa uwekaji nyasi bandia Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa na ule wa Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Mchikichini uliokuwa ukamilike 2024.
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omari Kumbilamoto ameishukuru Serikali kwa kuwa sikivu kuridhia uanzishaji wa soko hilo jipya la kisasa la uchomaji nyama linalofungua fursa kwa wakazi wa Vingunguti kujiingizia kipato na kukuza uchumi wao.
Ameongeza kuwa mradi huo unakwenda kusaidia kuinua uchumi kwa wakazi hao kwakuwa wamepata eneo zuri litalofanya wafurahie biashara zao ambapo awali walikuwa wakifanya biashara katika mazingira magumu ya tope na jua.