Latest Posts

SORAGA: KUNA HAJA ARUSHA NA ZANZIBAR KUSHIRIKIANA ZAIDI KIUTALII

Na Amani Hamisi Mjege.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mudrick Ramadhan Soraga amesema kuna haja Mkoa wa Arusha na Zanzibar kushirikiana zaidi kutokana na maeneo hayo mawili kuwa ya kimkakati katika kuvutia utalii.

Soraga amebainisha hayo alipokuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa msimu wa tisa wa maonesho ya Karibu Kili Fair 2024 yaliyofanyika Ijumaa Juni 07, 2024 kwenye viwanja vya Magereza Mjini Arusha ambapo amesema kuna mwingiliano mkubwa wa watalii wa Zanzibar na Arusha.

“Zanzibar na Arusha ni vitu viwili ambavyo huwezi kuvitenganisha, tunategemea sana utalii wetu. Watalii wengi wanaokuja Zanzibar kupitia ndege za kukodi au safari za ndege za umma mara nyingi huishia hapa Arusha, kwa hiyo kuna uhitaji mkubwa wa ushirikiano” Amesema Soraga.

Aidha Soraga amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda kwa juhudi anazozifanya za kuitangaza Arusha kiutalii kwani ndiye aliyewasilisha wazo la ushirikiano baina ya Arusha na Zanzibar kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi alipokuwa Arusha wiki chache zilizopita ili utalii wa maeneo hayo  mawili ukue zaidi.

Halikadhalika amesema Zanzibar imeweka mikakati ya kuongeza thamani kwenye utalii  ili kuvutia watalii kutalii kwa muda mrefu na kurudi kutalii kwa mara nyingine kwa kuwapa ladha tofuatitofauti za vivutio vya utalii.

“Hivi sasa, kiwango cha kurudi kwa watalii Zanzibar ni chini ya 20%, kwa hiyo ukichukua watalii kumi, ni wawili tu wanaorudi Zanzibar, hiyo si nzuri kwa Zanzibar na Arusha. Na tunatambua pengo lililopo ndiyo maana kupitia wizara yangu tumechukua juhudi za makusudi kubainisha umuhimu wa kuongeza thamani ya sekta kwa kuwekeza kwenye vivutio vyetu hasa vya turathi ikiwamo Stonetown lakini tuna zaidi ya Stonetown” Amesema Soraga.

Katika hatua nyingine Soraga amesema Zanzibar inatarajiwa kuzindua mradi wa kwanza wa uwekezaji katika visiwa vidogo vilivyoko Kisiwa cha Bawe tarehe 15 Juni, 2024 utakaozinduliwa na Rais Dkt. Hussein Mwinyi hivyo amewakaribisha washiriki wa onesho hilo kuhudhuria uzinduzi huo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!