Na Fredrizzo Samson – Tarime
Mkurugenzi Mtendaji wa Matiko Foundation na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Esther Nicholas Matiko, ametimiza ndoto yake kwa kuzindua rasmi Taasisi ya Matiko Foundation, iliyosajiliwa ngazi ya kitaifa.
Uzinduzi huo uliofanyika siku ya Jumanne tarehe 24 Septemba 2024 kwa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani Mara, walimu, wanafunzi, na wazee wa kimila, umeacha alama kubwa kutokana na malengo ya taasisi hiyo kushughulikia masuala mbalimbali ya kijamii.
Mgeni rasmi wa tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, aliwasili mapema katika ukumbi wa Blue Sky, akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mji.
Mtambi alipokea taarifa ya taasisi hiyo iliyosomwa na Katibu wa Matiko Foundation, Peter Michael Magwi ambaye pia ni Katibu wa Mbunge Matiko. Katika taarifa hiyo, viongozi na wajumbe waanzilishi wa taasisi hiyo walitambulishwa rasmi.
Katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Matiko Foundation, Esther Matiko alikabidhi mitungi midogo ya gesi ya kupikia 60 kwa walimu, pamoja na mashine moja kubwa ya ‘Photocopy’ na ‘Printing’ yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 12 kwa shule za sekondari za Tarime Mji. Mashine hiyo itahudumia shule zote za mjini, hasa katika kipindi cha mtihani.
Aidha, Matiko alikabidhi maboksi ya taulo za kike kwa wanafunzi, hatua ambayo itapunguza changamoto ya dharura kwa wanafunzi wa kike wanapoingia katika hedhi wakiwa shuleni.
Kwa habari kamili kwa njia ya video, tembelea YouTube channel yetu ya Jambo TV