Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, ametangaza mafanikio makubwa ya kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria nchini kwa asilimia 45 katika kipindi cha miaka saba, akisema kiwango hicho kimeshuka kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi asilimia 8.1 mwaka 2022.
Akizungumza siku ya Ijumaa Aprili 25, 2025 jijini Dodoma wakati wa kutoa tamko la kitaifa kuhusu maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani, Mhagama amesema pamoja na mafanikio hayo, Mkoa wa Tabora bado unaongoza kwa kiwango kikubwa cha maambukizi kwa asilimia 23. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Malaria Inatokomezwa na Sisi: Wekeza, Chukua Hatua – Ziro Malaria Inaanza na Mimi.”
Kwa mujibu wa takwimu alizotoa, mikoa inayofuata kwa viwango vya juu vya maambukizi ni Mtwara – 20%, Kagera – 18%, Shinyanga – 16% na Mara – 15%. Amesema mikoa iliyopungua maambukizi hadi chini ya asilimia 1 ni pamoja na Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Songwe, Mwanza, Dar es Salaam, Iringa, na Singida.
Katika hatua nyingine, Mhagama ametoa wito kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya malaria kwa kudhibiti mazalia ya mbu kwa kufukia madimbwi ya maji, kushiriki katika unyunyiziaji wa viuadudu vya kibaiolojia, kulala kwenye vyandarua vyenye dawa kila siku, kushona vyandarua vilivyochanika ili viendelee kuwa na ufanisi wa miaka mitatu, kuwahi vituo vya afya kwa uchunguzi wa malaria kabla ya kutumia dawa na kutumia dawa mseto ipasavyo na kumaliza dozi kama ilivyoelekezwa.
“Wajawazito kuwahi kliniki ili kupata huduma zote muhimu ikiwemo tiba kinga ya dawa ya SP na chandarua chenye dawa ili kujikinga na madhara ya ugonjwa wa malaria, watumishi wa afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma wahakikishe wanawapatia wajawazito na watoto chini ya mwaka mmoja vyandarua vyenye dawa ambavyo hutolewa na Serikali bila malipo,” Ameeleza Waziri Mhagama
Waziri amesema maadhimisho haya ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti malaria, kuangazia mafanikio, changamoto na kutoa elimu kwa jamii ili kufikia lengo la Tanzania isiyo na malaria.