
Na Helena Magabe – Tarime
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Tarime (TAFA), Mwalimu John Matiko, amemuomba Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Mhe. Michael Kembaki, kusaidia kufanikisha ukarabati wa Uwanja wa Shamba la Bibi ambao kwa sasa uko katika hali mbovu isiyofaa kwa shughuli za michezo.
Akizungumza wakati wa fainali ya mashindano ya Samia Cup, Matiko alisema uwanja huo hauna uzio, una mashimo, mabonde, na uchafu wa chupa zinazopasuliwa na watu walioko pembezoni mwa uwanja, hali inayohatarisha usalama wa wachezaji na wananchi wanaoutumia kwa mazoezi.
“Tunaomba usaidizi wa Mbunge kushirikiana na Halmashauri na wadau wengine. Uwanja huu si rafiki kabisa – walevi wanapasua chupa ovyo, wachezaji wanaumia, kuna mapungufu mengi,” alisema Matiko.
Amesisitiza kuwa uwanja huo unahitaji kufanyiwa maboresho makubwa yakiwemo kuweka nyasi bandia, kujenga uzio wa kuzuia wavamizi, kujenga vyoo, vyumba vya kubadilishia wachezaji na waamuzi na kuimarisha usalama kwa kufunga vichochoro
Matiko amebainisha kuwa Halmashauri tayari ina mpango mkakati wa kuufanyia kazi uwanja huo, lakini ucheleweshaji wa hatua za awali unakwamisha ushiriki wa wadau walioko tayari kusaidia.
Kwa upande wake, Michael Kembaki ameeleza kuwa jina la Samia Cup lilichaguliwa kuenzi mchango wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika maendeleo ya taifa, hususan katika kudumisha amani, na kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo kama vile soko la kisasa la zaidi ya Shilingi Bilioni 9.
“Ligi hii inahamasisha umoja, furaha na maendeleo. Rais wetu ameendelea kusimamia haki, amani na maendeleo katika kila sekta – hata michezo,” alisema Kembaki.
Mashindano hayo yamehitimishwa kwa burudani kutoka kwa msanii wa singeli Dulla Makabila aliyealikwa rasmi na Mbunge huyo, huku wakazi wa Tarime wakishiriki kwa shangwe na kucheza sigeli.
Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya Edward Gowele, alitoa zawadi mbalimbali kwa waamuzi, Kamati ya Michezo, Golikipa Bora na Timu Yenye Nidhamu. Aidha, timu zilizoshinda zilitunukiwa ni Turwa Cup (Mshindi wa Kwanza) – Shilingi Milioni 15, Nkende Cup (Mshindi wa Pili) – Shilingi Milioni 10, Bomani Cup (Mshindi wa Tatu) – Shilingi Milioni 5