Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, amethibitisha kuwa yuko mafichoni akihofia maisha yake. Katika mahojiano maalum na Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), Wine ameeleza kuwa kwa sasa anahifadhiwa na raia wa kawaida katika maeneo yasiyojulikana, huku kiongozi mwingine mkongwe wa upinzani, Dkt. Kizza Besigye, akiendelea kusota gerezani akiwa na hali mbaya ya kiafya.
Bobi Wine, ambaye amekuwa akiandamwa na ukandamizaji tangu uchaguzi wa mwaka 2021, amesema kuwa licha ya yeye kuwa mafichoni, familia yake imewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwa zaidi ya wiki moja sasa, ikizuiwa kutoka nje au kuwasiliana na watu. Hali hii inakuja huku kukiwa na shinikizo kubwa kutoka kwa Rais Yoweri Museveni na mwanawe, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni Mkuu wa Majeshi ya Uganda (UPDF).
Uhasama kati ya utawala uliopo na wapinzani umefikia kilele baada ya Jenerali Muhoozi (51), anayetajwa kuwa mrithi wa kiti cha urais, kutoa vitisho vya wazi vya kumuua Bobi Wine. Serikali imewachapa viongozi hao wa upinzani lebo ya “magaidi,” hatua ambayo wachambuzi wa siasa wanahofia inaweza kutumika kuhalalisha matumizi ya nguvu zaidi dhidi yao.
Uchaguzi wa Januari 15, 2026, uliompa Museveni ushindi wa muhula wa saba, umeendelea kupigiwa kelele na upinzani pamoja na waangalizi wa kimataifa wakidai kuwa uligubikwa na udanganyifu na vitisho vya kijeshi.