Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa umma na Utawala bora George Simbachawene ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kutupia jicho sekta ya ardhi inayoonekana kushamiri migogoro ya ardhi inayotishia ustawi wa wananchi na jamii kwa ujumla.
Kauli hiyo ameitoa Jumanne Juni 11, 2024 wakati akifungua mafunzo ya awali ya uchunguzi mwaka 2024 kwa maofisa wa TAKUKURU katika shule ya Polisi Tanzania iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Simbachawene amesema maeneo ya kutolea huduma nchini bado ni tatizo na sekta ambayo imeumiza nchi na kuleta migogoro mikubwa kwa familia na jamii ni sekta ya ardhi hivyo kuitaka taasisi hiyo kuitupia jicho kwa karibu na kuja na suluhisho.
“Msisitizo wangu, Mkurugenzi wa TAKUKURU tujikite zaidi maeneo ya kutolea huduma kwani kuna tatizo kubwa, wapo wenzetu wengine kwa kweli wanageuza sehemu za kutoa huduma kama ndiyo sehemu yao ya kupata kiinua mgongo na utajiri, na sekta ambayo imeiumiza nchi hii sana na imeleta migogoro mikubwa sana, kusumbua familia na jamii ni sekta ya ardhi” Amesema Simbachawene.
Pia, ameitaka TAKUKURU kushirikiana na vyombo vingine ikiwamo polisi na tume ya maadili kushughulika na wale wanaoghushi nyaraka za ardhi na kujipatia hatimiliki kinyume cha sheria
“Sasa hivi katika maeneo mengi watu wanalalamika, Waziri wa Ardhi (Jerry Silaa) anahangaika huko na huku, watu wameghushi nyaraka, kughushi ni jinai” Ameeleza Simbachawene.
Awali akitoa taarifa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP Salum Hamduni amesema maofisa uchunguzi wanaopatiwa mafunzo ya awali ya uchunguzi ni 310, wachunguzi wasaidizi 110 na watumishi 16 wanabadilisha kada.