Tamasha la Nyangumi (Whale Festival) 2024 limezinduliwa rasmi Agosti 28, 2024, na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda katika viwanja vya Mashujaa Park, Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhifadhi Mfawidhi wa Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma, Redfred Ngowo alisema lengo kuu la tamasha hilo ni kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo kusini mwa Tanzania ili kuweza kuongeza pato la mkoa na taifa kwa ujumla.

Ngowo aliongeza kuwa, licha ya kuwepo kwa vivutio vingi vya utalii, havitumiki ipasavyo katika kuongeza pato la mkoa, hivyo tamasha hilo limeandaliwa kwa jitihada za kuvitangaza vivutio hivyo ndani na nje ya nchi.
Tamasha hilo pia linalenga kujenga uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa rasilimali zinazohifadhiwa, pamoja na kutoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika sekta ya utalii kwa kujenga hoteli za kitalii na kuboresha huduma za utalii.
Hii itasaidia jamii kupata ajira na kuchochea mzunguko wa fedha kupitia mauzo ya bidhaa mbalimbali.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mwanahamisi Munkunda alisisitiza kuwa viongozi wanatekeleza maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Mtwara inatangazwa kwa utajiri wake mkubwa wa utalii.

“Niwaombe wananchi na wadau mbalimbali kushiriki kutangaza vivutio vilivyopo mkoani hapa. Pia, watumie mazao ya bahari ili kupata madini yenye faida kwa afya, kwani msimu wa Nyangumi huambatana na samaki wengi,” alisema Munkunda.
Naye Mhifadhi wa Bahari, Mussa Ally alieleza kuwa Nyangumi hupendelea kuja kwenye hifadhi hiyo kutokana na mazingira rafiki yanayokidhi mahitaji yao ya kujamiyana, kuzaana, na kulea.
“Pia, nyangumi husaidia kunyonya hewa ya ukaa ambayo inaleta athari kubwa kwa mazingira,” aliongeza Ally.