Latest Posts

TAMESO T YALAANI MATAPELI WANAOJIFICHA KWENYE SEKTA YA TIBA ASILI

Chama cha Waganga wa Tiba Asili Tanzania (TAMESO T) kimeeleza kusikitishwa kwake na kulaani vikali vitendo viovu vinavyoripotiwa kufanywa na watu wanaodai kuwa waganga wa jadi, ambao kwa hakika si wataalamu halali bali matapeli wanaojipenyeza katika sekta hiyo kwa lengo la kuwadanganya wananchi na kufanya udhalilishaji wa kingono.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa katika makao makuu ya TAMESO T mji mdogo wa Kibaigwa, wilayani Kongwa mkoani Dodoma, Katibu Mkuu wa TAMESO T, Lukas Joseph Mlipu, amesema matukio hayo yamezidi kuchafua taswira ya tiba asili licha ya kuwepo kwa juhudi kubwa za chama hicho katika kutoa elimu ya maadili ya kazi kwa waganga halali.

“Waganga wanaozingatia miiko ya taaluma hawawezi kushiriki katika vitendo vinavyokiuka maadili. Wanaofanya hivyo ni matapeli wanaoingia kwenye sekta hii kwa nia ya kutapeli na kudhalilisha,” amesema Mlipu.

 

Matapeli Wakemewa, Serikali Yatakiwa Kuingilia Kati

Mlipu ametolea mfano wa matukio ya udhalilishaji wa kingono yaliyoripotiwa mkoani Geita na kulaaniwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, kuwa ni ushahidi tosha wa namna matapeli wamejipenyeza na kuharibu taswira ya waganga wa jadi.

“Inasikitisha kuona watu hawa wanapokamatwa wanatangazwa kama waganga wa jadi wakati si kweli. Tunaiomba Serikali kupitia mamlaka zake mbalimbali kutupa ushirikiano ili kukomesha tabia hii,” alisisitiza Mlipu.

Aidha, ameeleza kuwa juhudi za TAMESO T katika kutoa elimu zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya ushirikiano mdogo kutoka kwa baadhi ya watendaji wa vijiji na kata, jambo linalochangia kuendelea kwa vitendo hivyo.

 

Wito kwa Waganga Halali na Jeshi la Polisi

Katibu huyo wa TAMESO T ametoa wito kwa waganga wote halali kushiriki kikamilifu kwenye semina na mafunzo ya chama hicho, ambayo hulenga kuwaimarisha katika utoaji wa huduma bora, salama na zenye kuzingatia miongozo sahihi ya tiba asili.

Pia ametoa mwito wa ushirikiano kati ya waganga na Jeshi la Polisi kwa kuwafichua watu wanaojifanya waganga na kutenda uhalifu ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

“Tujimudu, tushiriki semina, tuisaidie jamii kwa tiba salama na tuwafichue wahalifu wanaotuharibia kazi. Tunaposema tiba asili salama, maana yake ni tiba inayozingatia miiko, sheria na heshima kwa jamii,” amesema Mlipu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!