Theophilida Felician Arusha.
Chama cha tiba asili na tiba mbadala nchini TAMESOT kimeendelea na kampeni yake ya kuwafikia waganga wa tiba asili na tiba mbadala kwa lengo la kuwapatia elimu elekezi kuhusiana na huduma ya tiba asili.
Katibu mkuu wa chama hicho Bw Lukas Joseph Mlipu akiendelea na ziara mikoa kadhaa amekuwa mstari wa mbele katika kuielezea kwa upana tiba asili na tiba mbadala akiwapa mwanga mpana waganga ili waweze kutoa huduma yenye utaalamu zaidi kuliko ilivyozoeleka.
Katibu mkuu leo Tarehe 03 Machi amekutana na waganga wa mkoa Arusha akiwaelezea mada mbalimbali ikiwemo ya kuijengea misingi ya imani tiba asili ambapo amefafanua kuwa kumekuwepo na dhana potofu kwa waganga kuitwa wachawi pindi yanapotokea matukio yasiyofaa kwenye jamii jambo ambalo siyo sahihi kuhusisha tiba asili na imani ya kichawi.
Kiongozi huyo amesisitiza kuwa ili kuifuta dhana hiyo potofu ni vyema waganga wakafanya kazi ya tiba asili kwa kuzingatia misingi na miongozo ya taaluma hiyo kama inavyoelekezwa na baraza la tiba asili na tiba mbadala.
Hata hivyo waganga wa mkoa Arusha wamepongeza ujio wa katibu mkuu wa TAMESOT taifa ambapo wameahidi kuyazingatia mambo muhimu walionufaika nayo katika elimu hiyo elekezi.