Latest Posts

TAMKO LA TGNP  KULAANI KITENDO CHA UBAKAJI, ULAWITI NA UDHALILISHAJI WA BINTI, MKAZI WA JIJI LA DAR ES SALAAM ENEO LA YOMBO DOVYA

 

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) unalaani vikali kitendo cha ubakaji, ulawiti na udhalilishaji wa binti ambaye amejitambulisha kama mkazi wa Jiji la Dar es Salaam, eneo la Yombo Dovya. Tukio hili lilisambaa mitandaoni kuanzia tarehe 3 Agosti 2024 likionesha ukatili wa kijinsia uliotekelezwa na vijana watano waliodai kuwa wametumwa na kiongozi wao ambaye ni askari kufanya tukio hilo.

Tukio hili ni la kinyama na linakiuka haki za binadamu, utu, na hadhi ya binti huyu. Pia ni ukiukwaji wa misingi ya usawa wa kijinsia na haki ya kuishi bila hofu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 12(2) inasema: “Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.” Aidha, Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya mwaka 1981, kifungu cha 130(2)(e) kinasema: “Mtu yeyote anayefanya kitendo cha kubaka, atakuwa ametenda kosa na atawajibika kwa adhabu kali kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 131.” Kifungu cha 131(1) kinasema:”Mtu anayepatikana na hatia ya kosa la ubakaji atahukumiwa kifungo cha maisha jela au kifungo cha muda usiopungua miaka thelathini.”

Kwa kuzingatia hayo, TGNP inatoa wito kwa Serikali, Jeshi la Polisi, na mamlaka husika kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika wa tukio hili na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake bila kucheleweshwa. Tunataka kuona haki inatendeka haraka na kwa uwazi ili kutoa ujumbe kuwa vitendo hivi na vitendo vingine vya aina hii havitavumiliwa katika jamii yetu wala kufumbiwa macho.

Vilevile, TGNP inatoa wito kwa jamii nzima kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama ili kuleta wahusika mbele ya sheria na kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa mhanga wa tukio hili. Pia, tunatoa wito kwa mashirika ya kiraia na wadau wote kuendelea kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kijinsia na kudai mazingira salama kwa makundi yote haswa wanawake, wasichana, watoto na watu wanaoishi na ulemavu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!