Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia shirika la hifadhi za Taifa (TANAPA) katika kipindi cha mwaka 2020/2021 na mwaka 2022/2023 ilitumia jumla ya shilingi 144,268,404 kujenga nyumba ya Mganga na Nesi (mbili kwa moja) pamoja na kutengeneza samani kwa ajili ya kituo cha afya Hunyari, wilayani Bunda, mkoani Mara.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bunda (CCM) Boniface Mwita Getere aliyetaka kujua TANAPA itamalizia lini jengo la upasuaji katika kituo cha afya Hunyari kilichopo wilayani Bunda.
Akijibu swali hilo Kitandula ameongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TANAPA imeweka utaratibu wa kufadhili miradi ya ujirani mwema kwa maeneo yanayozunguka hifadhi za Taifa.
“Vilevile, ili kuendelea kunufaika na miradi ya ujirani mwema ambayo ni sehemu ya manufaa ya shughuli za uhifadhi na utalii, ninatoa rai kwa wananchi wa kijiji cha Hunyari, wilayani Bunda kutumia utaratibu uliowekwa na TANAPA katika kufadhili miradi ya ujirani mwema kwa kutuma maombi rasmi kuhusiana na umaliziaji wa jengo la upasuaji” Amesema Kitandula.