Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imelitaka shirika la umeme nchini (Tanesco) mkoani Mtwara kuhakikisha inarekebisha miundombinu ya umeme katika mkoa huo ili iendane na uzalishaji.
Akizungumza Septemba 9,2024 mkoani Mtwara, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini Kilumbe Ngenda amesema wameweza kuupandisha uzalishaji na kuwa na umeme mwingine wa ziada lakini miundombinu inawaangusha.
Amesema wanajua kazi kubwa inayofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali yake katika kuhakikisha mkoa huo wa mtwara unapata umeme wa uhakika.
“Tunajua hiyo kazi na tunampongeza Rais, tunaipongeza serikali, tunafahamu kazi hiyo ni ya tanesco kutwa kucha lakini kwa kuwa sisi tumepita hapa kwahiyo wananchi wa mtwara waseme kamati imepita na msisitizo wake mabadiliko wanayaona.”Amesema Ngenda
Hata hivyo ameipongeza tanesco kwa kufanikisha kuvifikia vijiji vyote 785 katika mkoa huo kwa kupitiwa na umeme wa Wakala wa Umeme Mijini na Vijijini (REA) kwani ni hatua mzuri na kubwa na ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Tuendelee kupelekea umeme huo vitongojini kama ambayo hatua ya wizara sasa hivi inavyosimami jambo hili”Amesema NgendaKamati hiyo iko mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na kazi zingine za kuishauri serikali pia kuangalia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na wizara ya nishati kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) ikiwemo ya Gesi Asilia iliyopo kijiji cha msimbati na Madimba kwenye halmashauri ya wilaya ya mtwara mkoani humo.
Miradi mingine ya maendeleo iliyotembelewa ikiwa ni pamoja na kituo cha afya msimbati kilichogharimu Sh milioni 700, kituo cha polisi na kupata fursa ya kuzungumza na wananchi wa kata ya Msimbati kwenye halmashauri hiyo walipokuwa katika miradi hiyo ya maendeleo kwenye kata hiyo.
Aidha amewaomba wananchi wa maeneo hayo kuwa wenye wajibu wa kutunza miradi hiyo ni wao ikiwemo ya Gesi Asilia ambayo inawanufaisha wananchi wa maeneo hayo na watanzania kwa ujumla.
Akiwa katika kituo hicho cha afya kwenye kata hiyo, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema fedha zilizojenga kituo hicho ni fedha za kurudisha kwa jamii zilizotolewa na TPDC.
Salma Mohamed, mkazi wa kijiji cha Msimbati, ameipongeza TPDC na serikali kwa ujumla kwa kuwekeza miradi hiyo ya maendeleo, ikiwemo kituo hicho cha afya, kwani kimewarahisishia upatikanaji wa huduma hiyo kwa urahisi na kuepukana na gharama kubwa za kufuata huduma hiyo katika kituo cha afya Likombe kilichopo Manispaa ya Mtwara Mikindani.