Latest Posts

TANROADS: BUNDA INAONGOZA WIZI WA TAA ZA BARABARANI MARA

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe ameibua wasiwasi juu ya ongezeko la wizi wa taa za barabarani, huku Wilaya ya Bunda ikitajwa kuwa kinara wa vitendo hivyo.

Akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara cha Mkoa wa Mara, meneja huyo amezitaka mamlaka husika kuchukua hatua za haraka ili kukomesha vitendo hivyo vinavyokwamisha jitihada za serikali katika kuboresha miundombinu na mazingira ya biashara hususan kwa wafanyabiashara wa vijijini.

“Pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kuhakikisha maeneo ya vijijini yanakuwa na mwanga wa kutosha usiku kwa ajili ya ufanisi wa shughuli za kiuchumi, bado tunakumbana na changamoto ya wizi wa taa za barabarani, jambo linalorudisha nyuma maendeleo,” amesema Maribe.

Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, amependekeza kuondolewa kwa taa katika maeneo yote yanayoshuhudiwa wizi huo, huku akitaka Maeneo ya Tarime Vijijini yapewe fursa ya kupata mwanga wa barabarani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya msako wa kina ili kubaini wahusika wa wizi huo na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

“Lazima tutokomeze kabisa vitendo hivi vya kuhujumu maendeleo. Ninaagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya msako mkali na kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema Kanali Mtambi.

Hatua hii inalenga kulinda miundombinu ya barabara na kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Mara wanaendelea kunufaika na miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!