Latest Posts

TANZANIA BARA NA ZANZIBAR ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA KISHERIA KATIKA KIKAO CHA WATAALAM

Kikao cha wataalam wa ushirikiano katika sekta ya sheria kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kimefanyika jijini Dar es Salaam, kikihusisha Wizara ya Katiba na Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Rais- Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Kikao hiki kililenga kujadili na kuimarisha ushirikiano wa kisheria kati ya pande mbili za Muungano sambamba na kuratibu mikutano ya kikanda na kimataifa kuhusu masuala ya sheria.

Akizungumza katika kikao hicho, Jane J. Lyimo, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Tanzania Bara, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kisheria kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema ushirikiano huo ni msingi wa kuimarisha masuala ya sheria kwa maslahi ya pande zote mbili za Muungano. Aliendelea kueleza kuwa kikao hicho kililenga kuhakikisha uratibu bora wa shughuli za kisheria, hususan kushiriki kwa pamoja kwenye mikutano ya kikanda na kimataifa.

“Ajenda ya kikao hiki ni kuimarisha uratibu wa shughuli za kisheria, hususani kushirikiana katika mikutano ya kikanda na kimataifa, ambayo ni muhimu kwa masuala ya kisheria na maendeleo ya kitaifa”, amesema.

Kwa upande wake, Ramadhani A. Jecha, Afisa Mipango kutoka Skuli ya Sheria ya SMZ, alibainisha kuwa mawasiliano na usimamizi wa pamoja kati ya pande hizo mbili ni muhimu katika kuboresha uwakilishi wa Tanzania kwenye masuala ya sheria kimataifa. Jecha alieleza kuwa ushirikiano wa karibu unatoa nafasi nzuri ya kuwasilisha masuala ya kitaifa kwa sauti moja na kwa ufanisi mkubwa.

“Tunaposhirikiana kwa karibu, tunakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuwasilisha masuala yetu kwa pamoja na kwa ufanisi kwenye mikutano ya kikanda na kimataifa,” amesema Jecha.

Naye Hanifa M. Selengu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Tanzania Bara, aliongeza kuwa vikao kama hivi vinaimarisha mshikamano wa kitaifa na kuwezesha Tanzania kutoa mchango mkubwa kwenye majukwaa ya kimataifa. Alisema ushirikiano wa pande hizi mbili unahakikisha kuwa Tanzania inachangia kikamilifu katika maendeleo ya sheria, siyo tu ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki, bali pia kimataifa.

Masuala muhimu yaliyojadiliwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya sheria ili iendane na mabadiliko ya kimataifa, kuweka mikakati madhubuti ya kushiriki kikamilifu kwenye mikutano ya sheria ya kimataifa, na kuhakikisha maazimio yaliyofikiwa yanatekelezwa kwa vitendo.

Kikao hiki kinatarajiwa kuwa mwanzo wa ushirikiano wa karibu zaidi katika sekta ya sheria, huku pande zote zikiweka ahadi ya kuhakikisha masuala ya kisheria yanashughulikiwa kwa pamoja na kwa mafanikio.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!