Uzinduzi wa Mpango wa Nishati Safi ya Kupikia Shuleni (Platform for Clean Cooking in Schools) katika Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30), Belem, Brazil umeweka msukumo mpya katika mapambano dhidi ya gesi joto duniani, huku Tanzania ikitumia nafasi hiyo kuimarisha mikakati ya matumizi ya nishati safi kama sehemu ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi.
Mpango huo uliobuniwa kama sehemu ya Ajenda ya Utekelezaji ya COP30- unapanua matumizi ya nishati safi kwenye taasisi za elimu duniani, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao ni chanzo kikuu cha ukataji miti na uzalishaji wa hewa ukaa (CO₂).
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP), zaidi ya watoto milioni 450 hupatiwa mlo shuleni kila siku duniani, jambo linalozifanya shule kuwa watumiaji wa pili kwa ukubwa wa nishati ya biomasi (mimea na wanyama) baada ya kaya. Katika nchi nyingi za Afrika, zikiwemo Tanzania, shule nyingi bado hutegemea kuni na mkaa, jambo linalosababisha uharibifu wa misitu, gesi joto na athari nyingine kwa afya.

Kwa mujibu wa wadau wa mpango huo akiwemo Sustainable Energy for All (SEforALL), mpito wa kupikia kwa nishati safi unaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa gesi joto, kwa sababu uko moja kwa moja katika mnyororo wa usalama wa chakula, afya na uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Damilola Ogunbiyi, Mkurugenzi Mtendaji wa SEforALL alisema, “Kama kila shule itakuwa na mfumo wa kupikia unaotumia nishati safi, tutakuwa tunalinda misitu, kuboresha afya na kupunguza hewa ukaa kwa kiwango kikubwa. Hili ni msingi wa mpito wa haki wa nishati.”
Upande wa Brazil, Dan Ioshpe, Balozi wa Tabianchi wa COP30, aliongeza kuwa mpango huu ni mfano wa hatua za mabadiliko ya tabianchi zinazofika moja kwa moja kwa wananchi: “Tunazungumzia mabilioni ya milo inayopikwa kwa kuni. Tukibadilisha hilo, tunabadilisha mustakabali wa mazingira na afya ya kizazi kijacho.”
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Peter Msoffe alisem Tanzania inachukua hatua mahsusi kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ikiwa ni sehemu ya kupunguza uzalishaji wa gesi joto unaotokana na ukataji miti na uchomaji wa nishati duni.

Alisema Serikali inatekeleza maelekezo kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kuacha kutumia kuni na mkaa, sambamba na kuongeza juhudi za upatikanaji wa nishati safi kwa gharama nafuu, akasisitiza kuwa dhamira ya Tanzania ni kuhakikisha kufikia mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Aliishukuru WFP na wadau wengine kwa kuanzisha programu za nishati safi shuleni nchini, akisema zinawafanya wanafunzi kuwa mabalozi wa tabia mpya zinazolinda mazingira na afya.
Kwa mujibu wa shirika la SEforALL, watu bilioni 2.1 duniani bado hawana upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, hali inayosababisha vifo vya mapema milioni 3.2 kila mwaka kutokana na kuvuta moshi wa majiko ya kienyeji.

Kwa upande wa mazingira, matumizi ya kuni na mkaa hutajwa kuwa chanzo kikuu cha uharibifu wa misitu, kupungua kwa bioanuwai, ongezeko la hewa ukaa (CO₂), athari za kiafya kwa watoto na wanawake. Stanlake Samkange wa WFP alisema, “Kila mtoto anapaswa kupata mlo wenye lishe bila kuathiri afya au sayari. Kupikia kwa nishati safi ni hatua ya msingi kuelekea hilo.”
Mpango wa Nishati Safi ya Kupikia Shuleni unatazamiwa kutekelezwa haraka, na tayari nchi 10 zimeanza hatua za awali. Lengo ni kufikia nchi nyingine 10 ifikapo mwaka 2026 na kufikia kiwango cha dunia ifikapo 2030.