Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema mabadiliko ya sera chini ya Rais wa Marekani Donald Trump yanaweza kusababisha Tanzania kuathirika, na kuwataka Watanzania kutumia rasilimali za ndani ili kujenga uchumi.
PM Majaliwa ameyasema hayo tarehe 6 Februari 2025 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole ambaye alitaka kufahamu kuhusu mipango ya serikali kulingana na mabadiliko ya sera za nje ya nchi ambazo zinatajwa kuathiri sera za elimu, afya na uchumi za Tanzania.
“Ni kweli kwamba serikali yetu inaheshimu sera za mambo ya nje na tunatekeleza mikataba kwa mujibu wa sera hizo kama ambavyo tumekubaliana na nchi hizo kwenye maeneo mbalimbali, tumeanza kuona nchi zenye uwezo mkubwa ikiwemo Marekani kubadilisha sera zao, na mabadiliko hayo yanaathiri baadhi ya nchi lakini pia hata nchi yetu inaweza kupata athari”, ameeleza Majaliwa, akisisitiza kuwa ni muhimu Tanzania kuendelea kuheshimu mabadiliko ya sera za nje kama ambavyo imekubaliana na jamii ya kimataifa.
Sambamba na hayo PM Majaliwa amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha uhusiano mzuri na nchi jirani.
“Muhimu kwetu ni kuhakikisha kwamba tunajiimarisha kwa kuwa na uwezo wa ndani ili kuhakikisha kwamba hatuendelei kuwa wategemezi, ni lazima tujiimarishe kwenye mipango yetu, bajeti zetu ziweze kumudu kutekeleza maeneo yote ikiwamo maeneo hayo ya afya pamoja na elimu”, amesema Majaliwa.