Latest Posts

TANZANIA KUTUMIA MADINI YA BETRI ZA MAGARI KUKUZA UCHUMI WA VIWANDA

Tanzania itatumia rasilimali ya madini ya kimkakati kukuza uchumi wa viwanda na kutoa mchango wake kwa dunia katika kutimiza malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs).
 
Hayo yameelezwa na Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji alipohihitimisha ziara yake ya kikazi nchini China alikohudhuria Mkutano wa Kimataifa ulioangazia namna ya kuharakisha malengo hayo.
 
Prof. Mkumbo ameeleza kuwa mkutano huo ulibaini kuwepo kwa changamoto zinazoyakabili mataifa mengi duniani, umasikini na mabadiliko ya tabia nchi yakiwa kitovu cha mjadala katika vikao mbalimbali vya mkutano huo.
 
“Tumeona katika mijadala kwamba, ili kuondoa umasikini tunahitaji uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu na teknolojia ya mawasiliano” Ameeleza Prof. Mkumbo.
 
Aidha amefafanua kwamba Tanzania ina nafasi ya kutoa mchango wake wa kutatua changamoto hizo kwa dunia hasa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
 
“Kuelekea 2030 dunia itabadilisha nishati, sisi Tanzania tuna madini yanayotumika kutengeneza betri za magari, hivyo tumetumia fursa hiyo kuwaalika wawekezaji kuwekeza kwenye viwanda vya kuzalisha betri, wakifanya hivyo, tutaisaidia dunia kutumia nishati safi, wao watakuwa wanatusaidia kupunguza umasikini, kwani hakuna nchi imeendelea bila kujenga viwanda” Amesema Prof. Mkumbo.
 
Naye balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya watu wa China, Khamis Mussa Omar ameweka wazi kuwa uhusiano wa China na Tanzania umeimarika sana katika sekta mbalimbali na sasa umetimiza miaka 60 na kuingia katika hatua mpya.
“Tangu tumeanzisha uhusiano na China miaka 60 iliyopita, tumekuwa na ushirikiano muhimu katika sekta za ujenzi wa miradi inayonufaisha jamii kama, kilimo, viwanda na miundombinu” Amesema Balozi Omar.
Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya watu wa China, Khamis Mussa Omar (Kulia) akiwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Lawrence Mafuru.
Kawa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Lawrence Mafuru, mijadala iliyoendelea katika mkutano huo imekuwa muhimu kwa Tanzania kuelekea katika uandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
 
“Mambo yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni ya kuzingatia katika mipango yetu na uandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, bila kufanya hivyo, tutajikuta tupo katika mtanziko kama dunia ilivyo leo kuhusu SDGs, Dira yetu isisahau kuwekeza kwenye elimu ya watu wetu ili watumia ujuzi na maarifa kuleta maendeleo, vile vile tumeona mijadala imesisitiza kuwa watu wenye afya ndio ufunguo wa uzalishaji, uwekezaji kwenye afya za watu wetu ni muhimu” Amefafanua Mafuru.
 
Imeelezwa kuwa mkutano huo pia umekuwa miongoni mwa vielelezo vya uhusiano mkubwa baina ya Tanzania na China, kwa kuwa mbali na Prof. Mkumbo kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la China (CDICA), alikuwa pia miongoni mwa viongozi walioalikwa kukutana na Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo Liu Guozhong.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!