Latest Posts

TANZANIA NA GUINEA BISSAU KUFANYA UTAFITI WA PAMOJA WA ZAO LA KOROSHO

Nchi ya Tanzania na Guinea Bissau zimekubaliana kushirikiana katika utafiti wa zao la korosho ili kuhakikisha wanaongeza uzalishaji na kuinua uchumi wa wakulima.
 
Makubaliano hayo yamefikiwa na viongozi wa nchi hizo, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais wa Guinea Bissau, Umaro Embalo aliyepo Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, Ikulu jijini Dar es Salaam.
 
Akizungumza na waandishi wa habari Rais Samia amesema Tanzania na Guinea Bissau ni miongoni mwa nchi zinazolima kwa wingi zao la korosho hivyo wamekubaliana kushirikiana kwenye utafiti ambao utaleta tija kwenye zao hilo na upangaji mzuri wa bei ya korosho.
 
“Tumejadiliana kwa kina kuhusu ushirikiano wetu ambao ulianza tangu wakati wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ila tumeamua kuweka mkazo katika kuhakikisha tunafanya utafiti wa zao la korosho na biashara ili kukuza uchumi wetu” Amesema Rais Samia.
 
Aidha Rais Samia amesema nchi hizo mbili zimepanga kushirikiana katika ukuzaji wa amani na usalama barani Afrika, ukuzaji wa biashara na uwekezaji, elimu, afya pamoja na uchumi wa buluu.
 
Rais Samia amesema eneo lingine ni maeneo huru ya uwekezaji ambapo Rais Embalo ataangalia maeneo ya Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) na Reli ya Kisasa ya SGR ili kuona mfano halisi wa jinsi miundombinu inavyounganisha nchi hizi mbili.
 
Katika hatua nyingine Rais Samia amesema wamekubaliana kushirikiana na nchi zingine za Afrika katika kuhakikisha bidhaa za kilimo za Tanzania na Guinea Bissau zinapata bei nzuri kwa kutengeneza umoja katika soko la dunia.
 
Aidha amesema bara la Afrika lipo mbioni kuhakikisha eneo huru la biashara linafunguka lengo likiwa kukuza zaidi kiwango cha biashara kati ya nchi za Afrika.
 
“Kuanzishwa kwa eneo hili pia kutachochea ukuaji wa viwanda, uongezaji wa thamani wa mazao yetu na kuleta ajira kwa vijana hivyo tumesema eneo hili huru la biashara tunalitumia ipasavyo” Amesema Rais Samia.
 
Kwa upande mwingine Rais Samia amesema Tanzania na Guinea Bissau zina maeneo makubwa ya Pwani hivyo watashirikana kwenye masuala ya uchumi wa buluu ikiwamo uvuvi, utalii wa fukwe na usafirishaji baharini.
 
Naye Rais wa Guinea Bissau, Umaro Embalo amesema Tanzania na nchi yake zikifanya kazi kwa pamoja zinaweza kuwa na amani ya kudumu na ustahimilivu wa kisiasa pamoja na kuwaletea maendeleo wananchi.
Aidha amewakaribisha wadau wa sekta binafsi nchini Tanzania kuwekeza Guinea Bissau kwani nchi hiyo ni lango muhimu la kuingia nchi zingine za Magharibi hasa kupitia eneo huru la biashara Afrika, na kumualika Rais Samia kutembelea nchini Guinea Bissau, mwaliko ambao Rais Samia ameukubali.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!