Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum ameshuhudia Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Korea zikisaini mkataba wa mkopo nafuu wa Shilingi bilioni 422.16 zitakazotumika kujenga Hospitali ya Rufaa ya Binguni, Zanzibar.
Mkataba wa Mkopo huo umesainiwa jijini Soeul, Korea Kusini tarehe 05 Juni 2024 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na kwa upande wa Korea umesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji Mwandamizi na Mjumbe wa Bodi wa Benki ya Exim Korea, Hwang Kiyeon.
Ujenzi wa Hospitali hiyo utahusisha majengo ya hospitali yenye vitengo vinne vya magonjwa maalumu yakiwemo ya akina mama na watoto, kituo cha mafunzo, nyumba za makazi ya wafanyakazi, ununuzi na ufungaji wa vifaa vya matibabu vya teknolojia ya kisasa, na usimikaji wa mfumo wa afya wa mawasiliano.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya ameeleza kuwa ujenzi huo utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa huduma bora za matibabu kwa watu wa Zanzibar, utapunguza idadi ya vifo kutokana na kuimarika kwa huduma bora za afya na matumizi ya vifaa vya kisasa, na utahamasisha utoaji wa mafunzo bora ya elimu ya afya kutokana na ujenzi wa kituo cha mafunzo kitakachokuwa na vifaa vya kisasa vya kujifunzia.
Mkopo wa bilioni 422.16 umeelezwa kuwa moja ya mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Korea iliyoanza Mei 31, 2024.