Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amesema mapato yatokanayo na shughuli za utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.3 Mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.9 Mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 200 kwa watalii wa kimataifa.
Balozi Dkt. Chana ameyasema hayo Jumatatu Mei 19,2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.
Aidha, amesema mapato yatokanayo na utalii wa ndani yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 46.3 Mwaka 2021 hadi Shilingi bilioni 209.8 Mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 353.1.
“Hatua hii imeifanya Tanzania kuwa nafasi ya tisa (9) duniani na kushika nafasi ya tatu (3) Barani Afrika kwa ongezeko la mapato ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya UVIKO-19.” Amesema.