Na Amani Hamisi Mjege.
Tanzania inaendelea kuonesha ukuaji thabiti wa uchumi, huku mfumuko wa bei ukiendelea kubaki ndani ya lengo la taifa la asilimia 5.
Kulingana na taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi Oktoba 03, 2024 na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Emmanuel Tutuba, Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) imetangaza kuwa hali hii inachangiwa na upatikanaji mzuri wa chakula, umeme wa uhakika, na utekelezaji wa sera imara za fedha.
“Mfumuko wa bei uliendelea kuwa tulivu, ndani ya lengo la nchi na vigezo vya mtangamano wa kiuchumi katika jumuiya za kikanda. Mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3 na 3.1 mwezi Julai na Agosti 2024, mtawalia, na unatarajiwa kuwa asilimia 3.2 katika robo ya nne ya mwaka 2024. Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa tulivu, ukichangiwa na kupungua kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, upatikanaji wa chakula cha kutosha na umeme wa uhakika, pamoja na utekelezaji wa sera madhubuti za fecha na kibajeti”, ameeleza Tutuba.
Aidha amesema kuwa uchumi wa taifa umekua kwa asilimia 5.6 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024, huku ukuaji ukitarajiwa kuendelea katika miezi ijayo. Tutuba amebainisha kuwa ukuaji huu umetokana na sekta za kilimo, ujenzi, usafirishaji, na fedha, ambazo zimekuwa nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania.
Katika sekta ya mikopo, ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi kwa asilimia 17.1 pia limechangia kuimarika kwa uchumi, huku mikopo chechefu ikiendelea kupungua na kufikia asilimia 3.9 kufikia Agosti 2024.
“Mikopo kwa sekta binafsi inatarajiwa kuendelea kuongezeka, sambamba na kuimarika kwa uchumi wa dunia na wa hapa nchini”, ameeleza Tutuba.
Aidha, ripoti ya kamati hiyo imebainisha kuwa mazingira ya kimataifa yanaendelea kuimarika, huku Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) likikadiria ukuaji wa uchumi wa dunia kwa asilimia 3.2 mwaka 2024.
Hali hii imetajwa kutarajiwa kuleta fursa zaidi kwa Tanzania kupitia uzalishaji wa ndani na biashara ya nje. Aidha kupungua kwa bei za mafuta na mbolea katika soko la dunia pia kumetajwa kusaidia kupunguza mfumuko wa bei nchini, hali inayoendelea kutoa nafuu kwa Watanzania.