Na Amani Hamisi Mjege.
Serikali ya Tanzania, kupitia Waziri wa Madini Anthony Peter Mavunde, imetangaza kufikiwa kwa muafaka kati ya Benki Kuu (BoT) na wadau wa sekta ya madini kuhusiana na uuzaji wa asilimia 20 ya dhahabu inayozalishwa kwa ajili ya akiba ya taifa.
Katika taarifa kwa umma ya tarehe 7 Oktoba 2024, Waziri Mavunde ameeleza kuwa mazungumzo na wachimbaji wakubwa, wa kati, wadogo, na wafanyabiashara wa dhahabu yamezaa matunda, hatua iliyotokana na kikao kilicholenga kushughulikia mgomo wa wanunuzi wa dhahabu mkoani Geita.
Katika mazungumzo hayo, pande zote zilikubaliana juu ya bei, malipo, na motisha ili kuwezesha utekelezaji wa kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini, kinachohusu kutenga asilimia 20 ya uzalishaji wa dhahabu kwa ajili ya akiba ya taifa kupitia Benki Kuu, kuwa wa mafanikio.
Waziri amefafanua kuwa bei itakayotumika ni ile ya dhahabu duniani, kama inavyotolewa na Tume ya Madini kila siku. Malipo kwa wauzaji wa dhahabu yatafanyika ndani ya saa 24 baada ya ripoti ya uchenjuaji wa dhahabu kupokelewa, huku Benki Kuu ikilipia asilimia 100 ya gharama za uchenjuaji.
“Benki Kuu italipia asilimia 100 ya gharama za kuchenjua dhahabu, asilimia 20 ya dhahabu inahusu mmiliki wa leseni ya uchimbaji wa madini na mfanyabiashara mkubwa wa madini”, ameeleza Mavunde.
Waziri Mavunde pia amebainisha kuwa wamiliki wa leseni za uchimbaji wa madini, wafanyabiashara wakubwa, na viwanda vya kuchenjulia dhahabu wanaweza kuuza kiasi chochote cha dhahabu kwa Benki Kuu.
Alisema, “Tumeweka motisha kwa wauzaji, ikiwemo kupunguza mrabaha kutoka asilimia 6 hadi 4, na ada ya ukaguzi kuwa asilimia 0 badala ya asilimia 1.”
Waziri Mavunde amesema kuwa hatua hizi zinalenga si tu kuboresha usimamizi wa akiba ya taifa bali pia kuhamasisha ukuaji wa sekta ya madini, huku akisisitiza kuwa mpango huo ni sehemu ya mkakati wa kuleta uwazi na ufanisi katika soko la madini, huku ukiimarisha uchumi wa taifa kwa kuongeza ushawishi wa Benki Kuu katika udhibiti wa dhahabu.
Benki Kuu inatarajiwa kuendelea kufanya kazi na sekta ya madini kuhakikisha utekelezaji huu unakuwa wa mafanikio na kuwa faida kwa wachimbaji wa madini, wafanyabiashara, na uchumi wa taifa kwa ujumla.