Latest Posts

TANZANIA YAJIBU VIKALI AZIMIO LA BUNGE LA ULAYA “HATUINGILIWI KATIKA HAKI ZETU ZA KIKATIBA”

Na Amani Mjege
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekanusha na kulaani vikali maudhui ya Azimio lililopitishwa na Bunge la Ulaya kuhusu mwenendo wa kesi zinazoshughulikiwa nchini, likielezwa kuwa limejengwa juu ya taarifa zisizo kamili na zinazopotosha.
 
Katika taarifa rasmi iliyotolewa siku ya Alhamisi Mei 8, 2025 na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tanzania imeeleza kushangazwa na tabia ya baadhi ya taasisi za kimataifa kushutumu maendeleo ya ndani ya nchi bila kupitia njia rasmi za kidiplomasia.
 
“Tanzania ni nchi huru inayoongozwa na Katiba na misingi ya utawala wa sheria. Masuala yote ya kisheria hushughulikiwa na Mahakama ambayo ni mhimili huru wa dola kwa mujibu wa sheria za nchi na viwango vya kimataifa, ambapo Serikali haitakiwi kuingilia mwenendo wa mashauri hayo. Hivyo basi, kauli au mapendekezo yanayohimiza kuingilia kati kwa Serikali katika mashauri yanayoendelea ni kinyume na misingi ya uhuru wa Mahakama kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kama inavyohimizwa na Umoja wa Ulaya,” imeeleza taarifa hiyo.
 
Serikali imefafanua kuwa tangu Machi 2021, chini ya falsafa ya 4R– Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi wa Taifa- mageuzi makubwa yamefanyika, ikiwemo kuundwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi mwaka 2024.
 
“Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba mafanikio yaliyopatikana, kama vile kuimarika kwa uhuru wa vyombo vya habari, ushirikishwaji wa kisiasa, mageuzi ya uchaguzi na juhudi za ujenzi wa amani kikanda, hayapatiwi uzito unaostahili, huku matukio machache ya kisheria yakipewa kipaumbele kisicho na uwiano”, imeelezwa.
 
Serikali pia imekanusha tuhuma zinazohusiana na haki za watu wenye mielekeo tofauti ya kijinsia, ikisisitiza kuwa “masuala hayo yanashughulikiwa kwa kuzingatia Katiba, sheria za nchi, maadili na mila za Kitanzania.”
 
Tanzania imekumbusha kuwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya utaendelea tu ikiwa utajengwa juu ya “heshima ya pande zote, uelewa wa mazingira ya kisheria na kitamaduni, na nia njema.”
 
Katika hitimisho lake, Serikali imesema: “Tanzania iko tayari kwa majadiliano ya wazi na ya kuheshimiana kwa maslahi ya maendeleo, lakini si kwa misingi ya shinikizo lisilo na uhalali.”
 
Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) lilitoa azimio rasmi lililolaani kukamatwa kwa Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nchini Tanzania, na kutahadharisha juu ya uwezekano wa hukumu ya kifo dhidi yake kutokana na mashitaka ya uhaini.
 
Katika Azimio la Bunge hilo lenye kumbukumbu namba 2025/2690 (RSP), wabunge wa Ulaya walionesha wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Tanzania, wakieleza kuwa mwaka 2025, Tanzania ilishushwa hadhi hadi daraja la “Not Free” (Isiyo Huru) katika ripoti ya Freedom House.
 
Bunge hilo lilieleza kuwa mashitaka ya uhaini nchini Tanzania yanaweza kupelekea adhabu ya kifo, jambo ambalo EU inalipinga vikali kwa hali yoyote ile. Bunge hilo limetoa wito kwa Serikali ya Tanzania kumwachia huru mara moja na bila masharti na kuhakikisha usalama wake pamoja na haki ya kupata uwakilishi wa kisheria.
 
Wabunge wa EU pia walilaani hatua ya serikali ya Tanzania kuizuia CHADEMA kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, pamoja na matukio ya kukamatwa kiholela kwa wapinzani, kufungwa kwa vyombo vya habari huru, vizuizi kwenye mitandao ya kijamii na matukio ya watu kutoweka kwa nguvu.
 
Katika mapendekezo yake, EU iliitaka Tanzania kusitisha mara moja unyanyasaji dhidi ya vyama vya upinzani, wanaharakati, waandishi wa habari na jamii za asili, kuruhusu uchunguzi huru dhidi ya polisi na matukio ya watu kutoweka kwa nguvu, kurejesha ushiriki wa CHADEMA katika uchaguzi mkuu, kufanya mazungumzo jumuishi na vyama vyote vya siasa kuhusu mageuzi ya uchaguzi, kuondoa sheria kandamizi za mitandao na vyombo vya habari, kufuta adhabu ya kifo na kubadilisha hukumu zote za kunyongwa.
 
EU imesisitiza kuwa misaada ya maendeleo kwa Tanzania kupitia mpango wa Global Gateway itazingatia masuala ya haki za binadamu, uhuru wa kujieleza na misingi ya haki katika mchakato wa kisheria.
 
Bunge la EU liliagiza azimio hili lipelekwe kwa Serikali na Bunge la Tanzania, Umoja wa Afrika, na kwa Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya (VP/HR).

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!