Latest Posts

TANZANIA YAJIPANGA KUSHIRIKI EXPO 2025, JAPAN

Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, imeeleza kuwa maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya Dunia (EXPO 2025) yanayotarajiwa kufanyika Osaka, Japan, yanaendelea kwa kasi. Maonesho haya yanachukuliwa kama jukwaa muhimu la kuutangaza uchumi wa taifa kimataifa na kutafuta fursa mpya za biashara, uwekezaji na ubia wa kimkakati.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, amesema kuwa EXPO ni jukwaa kubwa la kimataifa linaloleta pamoja mataifa mbalimbali kwa lengo la kutafuta suluhisho la changamoto zinazoukabili ulimwengu kupitia ubunifu, teknolojia na miradi ya maendeleo. Kaulimbiu ya EXPO 2025 inalenga kuchochea fikra mpya na ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto hizo.

EXPO hufanyika kila baada ya miaka mitano na hudumu kwa kipindi cha miezi sita. Huratibiwa na Shirikisho la Maonesho ya Dunia (Bureau of International Expositions – BIE), ambalo huratibu ushiriki wa nchi wanachama na pia kuchagua nchi mwenyeji. Kwa upande wa Tanzania, Shirika la Maendeleo ya Biashara (TanTrade) ndilo mwakilishi rasmi katika BIE.

Tangu mwaka 1967, Tanzania imekuwa mshiriki hai wa EXPO, ikiwa imeshiriki katika jumla ya maonesho tisa ya kimataifa, yakiwemo EXPO 2020 Dubai na EXPO ’70 Japan. Ushiriki wa mwaka huu unatarajiwa kuwa wa aina yake, ambapo taifa linakusudia kutumia jukwaa hili kukuza diplomasia ya uchumi, kuvutia wawekezaji, na kushirikiana na mataifa mengine katika maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia.

Kwa upande wa sekta binafsi, Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula, amesema kuwa ushiriki wa Tanzania katika EXPO 2025 utazingatia kutangaza bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, pamoja na kuonesha fursa zilizopo katika sekta mbalimbali kama afya, nishati, madini, utalii, kilimo, uchumi wa buluu, sanaa na utamaduni. Teknolojia na ubunifu vinatarajiwa kuwa nguzo muhimu za maonesho hayo.

Katika kuimarisha maandalizi, TPSF kwa kushirikiana na TanTrade, wameandaa Kongamano Kubwa la Biashara, Uwekezaji na Utalii litakalofanyika Mei 26, 2025. Kongamano hilo litawaleta pamoja wadau kutoka sekta mbalimbali, wakiwemo wawekezaji na makampuni kutoka Japan, kwa lengo la kujenga ushirikiano wa kibiashara, kubadilishana uzoefu, na kutia saini mikataba ya ushirikiano.

Kwa ujumla, Tanzania inatarajia kutumia EXPO 2025 kama jukwaa la kimataifa la kuinua hadhi ya taifa kiuchumi na kidiplomasia, sambamba na kuimarisha nafasi ya nchi katika soko la dunia.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!