Latest Posts

TANZANIA YAKANUSHA MADAI YA UKIUKWAJI WA HAKI GENEVA, YASEMA “TUNAZINGATIA KATIBA NA SHERIA ZA KIMATAIFA”

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswizi, Balozi Dkt. Abdallah Possi, amekanusha vikali madai yaliyotolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (EHAHRDN), akisisitiza kuwa Tanzania inazingatia ipasavyo Katiba yake pamoja na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu.

Akizungumza katika mkutano wa tano wa kikao cha 59 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Dkt. Possi amesema kuwa taarifa iliyotolewa na EHAHRDN ilikuwa na “taarifa potofu, zenye kupotosha na kuwasilishwa nje ya muktadha.”

“Tanzania inaheshimu uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, hata dhidi ya serikali, jambo ambalo hufanyika mara kwa mara kupitia mitandao ya kijamii,” amesema Dkt. Possi, akisisitiza kuwa taifa hilo ni demokrasia iliyokomaa.

Ameitaja historia ya Tanzania ya kufanya chaguzi za vyama vingi saba tangu kurejeshwa kwa mfumo huo kama ushahidi wa kujitolea kwa serikali kuhakikisha demokrasia na utawala wa sheria. Amesema kwa mujibu wa Katiba ya nchi, hakuna wakati wowote ambapo Tanzania imeshindwa kufanya uchaguzi kama inavyotakiwa.

Kuhusu watetezi wa haki waliotajwa na EHAHRDN, Dkt. Possi amesema walikiuka sheria za uhamiaji kwa kushindwa kutangaza madhumuni yao halisi ya kuingia nchini—hili likiwa ni hitaji la kawaida kwa mataifa mengi.

“Ingawa madai dhidi ya serikali ni ya kutia shaka, tunayachukulia kwa uzito mkubwa hasa yale yanayohusu mateso, ukatili wa kingono au ukiukwaji mwingine wa haki,” ameeleza Dkt. Possi, na kuongeza kuwa uchunguzi unaendelea na hatua zitachukuliwa iwapo itathibitika kuna ukweli.

Aidha amesema Tanzania imejizatiti kuhakikisha haki za binadamu na utawala wa sheria vinaendelea kuheshimiwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira huru na salama kwa vyama vyote vya siasa kufanya kampeni zao kwa amani.

Tamko hilo la Dkt. Possi limekuja kutokana na mashaka yaliyotolewa na baadhi ya wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya waandishi wa habari wa kigeni na wanaharakati waliofika Tanzania kufuatilia kesi ya Kiongozi wa Upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!