Licha ya changamoto kubwa zinazokumba uchumi wa dunia, Tanzania imefanikiwa kujiimarisha kiuchumi na kuingia kwenye orodha ya nchi kumi bora barani Afrika kwa Pato la Taifa (GDP) kwa mwaka 2024 ikishika nafasi ya 10, hiyo ni kulingana na ripoti mpya ya Mtazamo wa Uchumi wa Dunia (WEO) iliyotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) mwezi Oktoba, 2024.
Katika mkutano wa mwaka wa IMF uliofanyika Washington, Marekani, uchumi wa Tanzania unatarajiwa kufikia dola za Kimarekani bilioni 79.87 ifikapo mwisho wa mwaka 2024.
Ukuaji huu umeelezwa kuwa ishara ya mafanikio ya sera bora na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kusisitiza umuhimu wa maendeleo shirikishi katika sekta muhimu za kilimo, utalii, na viwanda.
Ukuaji wa uchumi wa Tanzania umeonekana kuwa endelevu na unaonyesha matumaini makubwa kwa miaka ijayo. Kulingana na makadirio ya IMF, ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) wa Tanzania ulifikia asilimia 5.1 mwaka 2023 na unatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 5.4 mwaka 2024, huku ikikadiriwa kufikia asilimia 6.0 mwaka 2025. Ukuaji huu unadhihirisha kuwa Tanzania inaimarisha misingi ya uchumi imara, licha ya changamoto za kimataifa kama vile mabadiliko ya tabianchi, bei za mafuta, na migogoro ya kikanda.
Kulingana na taarifa hiyo, Afrika Kusini inaongoza ikiwa na ukuaji wa uchumi wa Dola bilioni 403, ikifuatiwa na Misri (Dola Bil. 380). Kwa mataifa ya Afrika Mashariki katika orodha hiyo ukiachana na Tanzania, ni nchi ya Kenya ambayo ipo nafasi ya saba ikiwa na Dola bil. 116.3.

Kiujumla, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kupitia kwa Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Kristalina Georgieva linatabiri ukuaji wa asilimia 4.2 kwa Afrika ifikapo mwaka 2025, huku likiona ukuaji thabiti lakini wa polepole barani humo.

“Eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara linaonyesha viwango vya ukuaji ambavyo viko thabiti mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliopita, takriban asilimia 3.6, na tunatarajia kuongezeka hadi takriban asilimia 4.2 mwakani,” alisema Pierre-Olivier Gourinchas, Mchumi Mkuu wa IMF.
Kulingana na takwimu za IMF kuhusu uchumi wa nchi zinazoendelea na masoko yanayokua, Tanzania imeweza kudhibiti viwango vya mfumuko wa bei ukilinganisha na baadhi ya nchi jirani. Kwa mfano, mwaka 2024, nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zinatarajia mfumuko wa bei wa juu zaidi, kama vile Angola (asilimia 18.1) na Ghana (asilimia 19.5), wakati Tanzania inaendelea kusimama imara na viwango vya wastani vya mfumuko wa bei.
“Mfumuko wa bei unadhibitiwa katika baadhi ya nchi… na kufikia viwango karibu na malengo, lakini nusu ya nchi bado ziko mbali sana na malengo hayo, na theluthi moja bado zinakabiliwa na mfumuko wa bei wa tarakimu mbili,” alisema Jean-Marc Natal, Mkuu wa Idara ya Utafiti, IMF.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya IMF, ukuaji wa uchumi katika nchi za Afrika hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara umekuwa wa polepole lakini endelevu. Ukuaji huo unakadiriwa kufikia asilimia 4.2 ifikapo mwaka 2025, kutoka asilimia 3.6 mwaka 2024. Ripoti hiyo inaeleza kuwa ukanda huu umekumbwa na changamoto mbalimbali kama vile mabadiliko ya tabianchi na migogoro, hali inayofanya ukuaji wa uchumi kuwa wa kusuasua katika baadhi ya nchi. Hata hivyo, Tanzania imeweza kuvuka vikwazo hivyo na kuendelea kujenga uchumi wa kisasa unaojumuisha sekta mbalimbali muhimu kama kilimo, viwanda, na utalii.