Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema ni vyema Tanzania ikatumia fursa zilizopo katika muunganiko wa Afrika Mashariki ili kujiimarisha kiuchumi, na kwamba Afrika Mashariki siyo Jumuiya tu bali ni shirikisho la kufungua fursa nyingi za kiuchumi ambazo zikitumika vyema zitaleta tija kwa Taifa.
Othman ametoa kauli hiyo Ijumaa Agosti 09, 2024 alikutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki ulioongozwa na Waziri katika Wizara hiyo Balozi Mahmoud Thabit Kombo, uliofika Ofisini kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Migombani, mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja kwa lengo la kujitambulisha baada ya mabadiliko ya hivi karibuni aliyoyafanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya baraza lake la mawaziri.
Aidha, Othman amewaelekeza viongozi wanaosimamia wizara hiyo kuzitumia fursa zilizopo katika taasisi za kimataifa ili kuendana na kasi za kimaendeleo ulimwenguni.
“Zipo Taasisi kama WIPO, zinazobeba fursa nyingi ndani yake, ambazo Mataifa ya Asia na Ulaya wanazitumia vilivyo kujinufaisha, ila kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla bado tupo nyuma sana, tukizingatia hili ni jambo adhimu kwa mustakbali wa maendeleo ya nchi yetu “, ameeleza Othman.
Aidha Othman amewahimiza wahusika na watendaji wa wizara hiyo kutoa elimu kwa jamii za wazawa na hata wageni, juu ya mambo ya msingi yanayoihusu Serikali ya Muungano ili kuondoa mkanganyiko, sambamba na kuwajengea uelewa mpana wananchi katika kuelewa haki zao, na pia maeneo sahihi ya kupata huduma kwa wakati.
Akieleza suala la tija kupitia sekta za utalii kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, Othman amehamasisha kuwepo kwa kumbi za mikutano zenye hadhi ya kimataifa ili kuvutia harakati za mataifa ya kigeni, kwa lengo pia la kulinufaisha taifa.
Naye, Waziri Mahmoud ameahidi kwamba wizara yake hiyo mpya itafanya kazi kwa karibu na viongozi wakuu pamoja na watendaji wote waliopo Zanzibar ili kuleta ufanisi na kuhakikisha wanayafikia malengo kwa ajili pia kuitangaza zaidi nchi katika jamii ya kimataifa.
Aidha, Mahmoud ambaye ameshika wadhifa huo hivi karibuni akitokea kuwa balozi wa Tanzania nchini Italia ameahidi kuitendea kazi miongozo na mashauri yote aliyopewa kwa masilahi ya Taifa.
Viongozi mbalimbali wamehudhuria katika kikao hicho wakiwemo Manaibu Waziri katika Wizara hiyo, Cosato Chumin a Denis Lazaro, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje Zanzibar Balozi Silima Kombo Haji pamoja na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Ilyasa Juma Pakacha.