Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), imetafiti aina mbalimbali za mbegu zinazokabiliana na wadudu, magonjwa pamoja na mabadiliko ya tabia nchi ikiwamo ukame.
Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Thomas Bwana amesema hayo katika kilele cha maadhimisho ya wakulima, wafugaji na wavuvi jijini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari ambapo amesema taasisi hiyo inafanya utafiti huo wa mbegu ili kutatua changamoto zinazowakabili wakulima zinazotokana na magonjwa, wadudu na hali ya hewa.
“Sasa hapa tunakuja kuonyesha aina mbalimbali za teknolojia ambazo wameziandaa TARI kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za wakulima ikiwa ni pamoja na changamoto za rutuba ya udongo, wadudu waharibifu, lakini changamoto za magonjwa”, amesema Bwana na kuongeza,
“Tuna aina mbalimbali za mbegu bora za migomba, mbegu za jamii ya mikunde lakini tuna mbegu za mpunga, mahindi na korosho”.
Amesema taasisi hiyo imekua ikitafiti mbegu bora ambazo zinakinzana na magonjwa na zenye mazao mengi zaidi ili kuongeza tija kwa wakulima.
“Lakini pia kuna tekinolojia nyingine kama ile ya kitalu mkeka hiyo inasaidia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, teknolojia hii ya kitalu mkeka mkulima anaweza kuandaa mbegu hata nyumbani, inasaidia kukimbizana na mvua ambazo zinakua zinabadilika basilica,” amesema.