Latest Posts

TARIME MJI YAPATA HATI SAFI MIAKA MITANO MFULULIZO, RC MTAMBI APONGEZA, ATAKA KASI ZAIDI

Na Helena Magabe-Tarime.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi, ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa mafanikio ya kupata hati safi kwa miaka mitano mfululizo kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini ameitaka kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kufikia malengo ya mwaka wa fedha.

Akizungumza Juni 5, 2025, katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani, kilichoitishwa kwa ajili ya kujadili taarifa ya CAG, RC Mtambi alisema hadi kufikia Mei 31, 2025, Halmashauri hiyo ilikuwa imekusanya shilingi bilioni 2.6, sawa na asilimia 73 ya lengo la bilioni 3.6.

“Ingawa Mwenyekiti wa Halmashauri amejaribu kutoa maelezo, hali ya makusanyo si ya kuridhisha. Ni lazima mjipange vizuri kwenye siku chache zilizobaki ili kufikia malengo kabla ya Juni 30,” alisema Mtambi.

RC Ataka Mpango wa Maandishi wa Kukamilisha Mapato

Kanali Mtambi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri, Bw. Gimbana Ntavyo, kuwasilisha kwake tarehe 9 Juni 2025, taarifa ya maandishi inayoonesha mikakati ya kukamilisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha.

Aidha, aliwataka madiwani kushirikiana na menejimenti kubuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia kikamilifu vile vilivyopo ili kufanikisha miradi ya maendeleo na shughuli za uendeshaji wa Halmashauri.

Maagizo Maalum kwa Menejimenti ya Halmashauri

RC Mtambi alitoa maagizo sita kwa Halmashauri hiyo, yakiwemo:

  1. Asilimia 10 ya mapato ya ndani iendelee kutengwa kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
  2. Madeni ya miaka ya nyuma yakusanywe kikamilifu ili kuimarisha mfuko wa maendeleo.
  3. Menejimenti isijihusishe na maamuzi bila baraza pindi litakapovunjwa.
  4. Idara ya manunuzi itumie mfumo wa kielektroniki wa NeST kama taratibu zinavyotaka.
  5. Usimamizi wa mapato uimarishwe mara moja.
  6. Mipango ya maendeleo izingatie vipaumbele vya wananchi.

Mwenyekiti wa Halmashauri: Tumejipanga Kutekeleza Maagizo

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Mhe. Daniel Komote, alisema maagizo yote ya Mkuu wa Mkoa yamepokelewa na yatafanyiwa kazi, akieleza kuwa hadi kufikia Juni 30, 2025, mapato ya ndani yatakuwa kwenye viwango vinavyotakiwa.

Aidha, alimshukuru Mkurugenzi na menejimenti kwa ushirikiano unaowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo licha ya ukosefu wa miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

“Pamoja na changamoto, Halmashauri yetu imeweza kujenga shule mpya, zahanati, vituo vya afya na kumalizia ujenzi wa taasisi mbalimbali kila mwaka kwa kutumia mapato ya ndani,” alisema Komote.

Omba Hospitali Ipandishwe Hadhi

Komote pia aliomba Hospitali ya Halmashauri kupandishwa hadhi, akieleza kuwa inahudumia siyo tu kata za Mji wa Tarime, bali pia wagonjwa kutoka Halmashauri ya Tarime Vijijini na hata wilaya jirani ya Rorya.

“Uhitaji wa dawa ni mkubwa sana, hali ambayo husababisha dawa kuisha ndani ya wiki moja hadi mbili,” alisema.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!