Latest Posts

TEF YALAANI KAULI ZA KULIINGIZA JESHI KWENYE SIASA

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limelaani vikali kauli na video zilizozagaa mitandaoni zikionyesha watu wanaodaiwa kuwa wanajeshi wakihamasisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujiingiza katika siasa kupitia njia ya mapinduzi.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deodatus Balile imesema matamshi hayo ni hatari kwa usalama wa taifa na yanakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inatenganisha jeshi na shughuli za kisiasa.

Katika hatua nyingine, TEF imepongeza hatua ya haraka ya JWTZ kutoa taarifa kwa umma ndani ya muda mfupi kukemea matukio hayo, likieleza kuwa hatua hiyo inaonyesha uadilifu, weledi na utii wa jeshi kwa misingi ya Katiba.

Katika taarifa yake, JWTZ lilieleza kuwa linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa uaminifu, utii na uhodari kwa kuzingatia kiapo chake cha kijeshi.

Jukwaa hilo la Wahariri Tanzania limesema hatua hiyo inaonyesha kwamba jeshi linaendelea kuwa taasisi imara, yenye kuheshimu mipaka ya kikatiba na kutojihusisha na siasa.

Balile amesema tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Tanzania imeendelea kudumisha amani na utulivu, hata katika nyakati za joto la kisiasa, kwa sababu wananchi na taasisi zake wamekuwa waumini wa demokrasia huku akisisitiza kuwa nchi nyingi zilizopitia mapinduzi zimejikuta zikikumbwa na machafuko, mateso, uharibifu wa mali na kudhoofika kwa taasisi za dola.

“Tanzania imepata majaribu ya mapinduzi mwaka 1964, 1969 na 1982, lakini kwa hekima ya viongozi na umoja wa wananchi, taifa letu liliweza kushinda majaribu hayo na kujenga mfumo thabiti unaolitenganisha jeshi na siasa,” amesema Balile.

Amevitaka vyama vya siasa visijihusishe kwa namna yoyote na fikra za mapinduzi kama njia ya mkato kuingia madarakani, na badala yake vijenge vyama imara vinavyoshindana kwa sera na kuamini katika nguvu ya sanduku la kura. Ameonya pia kuwa vyama vya siasa visikae kimya mbele ya kauli zenye mwelekeo wa uchochezi, bali vizilaumu waziwazi kwa nia ya kulinda amani, umoja na maisha ya Watanzania.

Balile amesema mitandao ya kijamii imekuwa chanzo kikuu cha upotoshaji, ambapo baadhi ya watumiaji wamekuwa wakisambaza taarifa zisizo sahihi, picha zenye udanganyifu na matusi dhidi ya viongozi wa umma. Ameongeza kuwa hali hiyo inahatarisha amani na mshikamano wa taifa, na kuwataka Watanzania wawe makini na wachunguze ukweli kabla ya kusambaza taarifa wanazopokea.

“Tunawasihi Watanzania tuwe makini na tuchunguze ukweli kabla ya kusambaza taarifa zinazotufikia kwenye simu zetu. Wenye mitandao watangulize maadili, uzalendo na uwajibikaji,” amesema.

Amesema Tanzania imejengwa juu ya misingi ya amani, umoja na mshikamano, na njia pekee ya kuendeleza uongozi ni kupitia demokrasia na ridhaa ya wananchi. Ameongeza kuwa TEF linaendelea kuunga mkono juhudi za JWTZ na taasisi nyingine za ulinzi na usalama katika kulinda Katiba na kudumisha amani ya taifa.

“TEF tunakemea vikali kauli za kuchochea mapinduzi, tunalipongeza JWTZ kwa uaminifu wake kwa Katiba, na tunawasihi Watanzania wote kulinda amani na umoja wa taifa letu muda wote. Mungu ibariki Tanzania,” amesema Balile.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!