

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) likiongozwa na Mwenyekiti wake , Deodatus Balile, Machi 12, 2026 limetembelea mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji sita vilivyopo ukanda wa Ziwa Nyasa wilayani Ludewa mkoani Njombe, mradi unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 3.1 ulianza kutekelezwa Julai 13, 2025 na unatarajiwa kukamilika Aprili 13, 2026, ukilenga kuwapatia huduma ya umeme wateja wa awali takribani 160.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Msimamizi wa Miradi wa REA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Dastan Kalugira, amesema mkandarasi wa mradi huo, Suma JKT, tayari amekamilisha kazi ya kusimamisha nguzo zote 105 zinazohitajika katika vitongoji vyote vinavyonufaika na mradi huo.
Amesema hatua iliyobaki ni kuvuta waya ili kukamilisha miundombinu ya usambazaji wa umeme kabla ya wananchi kuanza kupata huduma hiyo.
“Baada ya kukamilika kwa mradi huu, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) litaendelea kuwaunganisha wateja wapya kwa gharama za REA,” alisema Kalugira.
Ameongeza kuwa mradi huo ni wa kipekee kutokana na mazingira ya milimani katika eneo hilo, hali iliyosababisha changamoto katika usafirishaji wa vifaa na utekelezaji wa kazi.
Mhandisi Kalugira pia amefafanua kuwa, ingawa mradi huo upo katika Mkoa wa Njombe, baadhi ya vitongoji vinne vilivyopo upande wa ufukwe wa Matema wilayani Kyela mkoani Mbeya vitaunganishwa na umeme kutoka upande huo kutokana na ugumu wa kuvifikia kupitia Njombe.
Vitongoji vitakavyonufaika na mradi huo ni Kitewele na Kimata vilivyopo wilayani Ludewa, pamoja na Kigulu, Chanjale, Lumbira na Nkanda vilivyopo upande wa Matema wilayani Kyela mkoani Mbeya.
Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi huo, Yassin Seleman, amesema utekelezaji wa mradi ulikumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo jiografia na mazingira ya eneo hilo ikiwemo milima mikali na hali mbaya ya hewa hasa mvua.
Amesema katika baadhi ya siku walilazimika kusafirisha nguzo moja tu kwa siku kwenda eneo la mradi kwa kutumia trekta kutokana na ugumu wa njia.
“Pamoja na changamoto hizo tumefanikiwa kusimamisha nguzo zote 105 na sasa tunasubiri vifaa kwa ajili ya kuvuta waya,” alisema Seleman.
Aidha amesema mradi huo umechangia kutoa ajira kwa wananchi wa eneo hilo, ambapo jumla ya watu 80 walipata fursa ya kufanya kazi wakati wa utekelezaji wake.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini unaonesha namna mchango wa wananchi kupitia asilimia tatu ya mapato ya mauzo ya umeme inayokwenda REA unavyotumika kuleta maendeleo.
“Leo tunashuhudia vitongoji sita vilivyopo katika mazingira magumu vikielekea kupata huduma ya umeme. Hii inaonesha wazi kuwa michango ya wananchi inarejea kwao kwa njia ya maendeleo,” alisema Balile.
Balile amesitiza kuwa, maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana bila wananchi kushiriki kugharamia miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa takwimu za Mkoa wa Njombe, kuna jumla ya vijiji 381 na vyote tayari vimeunganishwa na huduma ya umeme. Kati ya vitongoji 1,833 vilivyopo mkoani humo, vitongoji 1,249 tayari vimepata umeme huku vitongoji 584 vikiwa bado havijafikiwa na huduma hiyo.