Kwa takribani miaka nane (08) sasa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umekuwa na kawaida ya kuwa na majukwaa mbalimbali ikiwamo jukwaa lijulikanalo kwa jina la Kijiwe cha Kahawa kwa lengo la kujenga nguvu za pamoja ili kuleta chachu ya mabadiliko chanya kisera, kiutendaji na kifikra.
Hayo yamesemwa Alhamisi Juni 13, 2024 na Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Gemma Akilimali akiongea katika ufunguzi wa jukwaa hilo ambapo amesema jukwaa hilo limefanikiwa kuwaleta pamoja wadau mbalimbali na kutoa fursa ya kusikiliza hotuba ya hali halisi ya uchumi pamoja na kutathimini bajeti kuu ya serikali 2024 /2025 kwa mtazamo wa jinsia kwa kuzingatia matarajio ya wananchi.
Aidha Bi. Akilimali amesema kuwa jukwaa hilo linatumika pia kama nyenzo ya kuwakutanisha wadau kwa ajili ya kuunganisha nguvu za pamoja katika kudai utengaji wa bajeti kwa mlengo wa kijinsia ambapo nguvu hizo zimeanza kuzaa matunda.
“Moja ya hatua zilizopigwa ni pamoja na uingizwaji wa bajeti za kijinsia katika malengo matatu ya kimkakati kati ya malengo matano yaliyopo kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo” Amesema Bi. Akilimali.
Pamoja na kueleza mafanikio, Gemma ameeleza kuwa kuna changamoto ya utengwaji hafifu wa rasilimali zinazoweza kuchangia kufikia usawa wa kijinsia na utolewaji wa rasilimali fedha aidha kidogo au iliyo nje ya muda jambo ambalo linachangia kufifisha azma ya kufikia usawa wa kijinsia.
“Bado hatujaweza vya kutosha kuingiza masuala ya kijinsia kwenye sheria na sera hii ni kutokana kukosekana mpango mzuri na uratibu kutoka Wizara ya Fedha” Amesema Gemma.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi amesema bajeti kuu ya serikali ya mwaka 2024/2025 imekuja katika muktadha wa kipekee katika kipindi ambacho nchi inatengeneza dira ya Taifa ambayo itaamua hatma ya maisha ya wananchi wa Tanzania ya miaka 25 ijayo.
“Bajeti ni kitu cha muhimu sana, na ni lazima wananchi watoe maoni na sauti zao. Kufuatia hilo, TGNP tumeandaa jukwaa hili (Kijiwe cha Kahawa) tukifahamu umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika michakato ya bajeti kwa kuwa bajeti inatoa dira ya mwaka ya maisha ya watu. Tunatamani wananchi washiriki michakato yote hiyo” Amesema Liundi.
Aidha Liundi ametoa rai kwa serikali kuangalia suala la utoshelevu wa rasilimali zote ambazo zitawawezesha wanawake wengi kushiriki katika uchaguzi ili waweze kutoa sauti zao kupitia uwakilishi wao kwenye nafasi mbalimbali za uongozi kinyume na sasa ambapo takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi ngazi za Serikali za Mitaa kuwa ni ndogo.
Wakiongea kwa nyakati tofauti Hellen Sisya ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Her Education na Christina Silas kutoka Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) wamesema matarajio yao ni kuona bajeti ya mwaka 2024/2025 inaleta unafuu kwa vijana na makundi maalumu pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Dhima ya Kijiwe cha Kahawa mwaka huu inasema ” Kuelekea Bajeti Kuu ya Serikali 2024 /2025, Wekeza Katika Usawa wa Kijinsia, Ushiriki wa Wanawake katika Uongozi na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayogusa makundi yote”.