Latest Posts

TGNP YASHAURI VIJANA NA WANAWAKE WAPEWE MOTISHA ZA KIKODI NA MITAJI ILI WAJIAJIRI

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umependekeza serikali kutoa motisha na hamasa za kikodi na mitaji, kufungua fursa na kulegeza masharti ya kuanzisha biashara katika sekta zinazoendelea kukua kwa kasi zaidi ili kundi kubwa la nguvu kazi ya taifa ambalo ni vijana na wanawake waweze kujiajiri au kuajiriwa.

Pendekezo hili limeelezwa katika tamko la TGNP lililotolewa hivi karibuni likihusu hotuba ya hali ya uchumi na Bajeti ya Taifa zilizosomwa Alhamisi tarehe 13 Juni 2024, na Waziri OFisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Kitila Mkumbo pamoja na Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba, likiwa na lengo la kuwasilisha muhtasari wa uchambuzi uliofanywa na wanamtandao kuhusu hotuba hizo kwa kuzingatia mahitaji na vipaumbele vya kijinsia.

Katika uchambuzi huo, TGNP imeainisha baadhi ya hatua chanya ambazo nchi ya Tanzania inaendelea kupiga katika kuondoa tofauti na kuziba mapengo ya kijinsia katika sekta na huduma mbalimbali ikiwamo uanzishwaji wa mfuko wa dharura wa kutengeneza miundombinu ya barabara zilizoharibika.

“Uharibifu wa barabara umekuwa ukisababisha ufikiwaji wa huduma za afya kwa mama wajawazito, wagonjwa mahututi kuwa ngumu pia zimekuwa zikihatarisha usalama wa watoto na wanafunzi wanaoishi vijijini wasiweze kufika au kwenda shule wakati wa mvua nyingi. Barabara zilizoharibika zimekuwa pia zikichangia wakulima hasa wanawake kushindwa kufikisha bidhaa zao masokoni kwa wakati na wakati mwingine kushindwa kabisa kwa sababu ya gharama za usafiri kuwa juu wakati wa mvua hivyo kulazimika kuuza mashambani kwa bei ndogo” Limeeleza tamko hilo.

Hatua nyingine chanya ni kuendelea kutoa unafuu wa ushuru wa forodha kwa kutoza kiwango cha asilimia 0 kwenye malighafi za kutengenezea taulo za kike pamoja na nepi za watoto kama sehemu ya makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Hii inaonesha nia ya kuendelea kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa taulo za kike hususani kwa ajili ya wasichana wanaotoka katika kaya maskini lakini pia katika kuhakikisha wanawake na wasichana hawaadhibiwa kwa kulipa kodi ya ziada sababu ya hitaji hili linalotokana na maumbile ya kibaolojia” Imeeleza TGNP.

Pamoja na hatua hizo, TGNP imeona kuna haja ya mambo kadhaa kuboreshwa ikiwamo eneo hilo la taulo na nepi za Watoto, ikielezwa kuwa hatua iliyopigwa haitoshi kuhakikisha kuwa gharama za taulo hizi anazolipa mtumiaji wa mwisho zinapungua kwani serikali haijawa na mkakati wa kuhakikisha kuwa wasambazaji na wauzaji wa bidhaa hizi wanashusha bei kulingana au sawasawa na kupungua kwa gharama za uzalishaji ambazo zinakuwa zimejitokeza baada ya kupewa unafuu wa ushuru wa forodha.

Jambo lingine ni kwenye dadi ya vijana wanaofaidika na mikopo ya kilimo kupitia programu ya BBT ambayo ni kidogo ukilinganisha na uhitaji uliopo licha ya kwamba kulingana na hotuba ya hali ya uchumi mikopo katika sekta ya kilimo iliongezeka kwa kasi kubwa katika mwaka 2023/24.

Kulingana na changamoto zilizoainishwa kwenye tamko hilo, TGNP imeshauri mambo kadhaa ikiwamo kuongeza jitihada za uwekezaji katika kusaidia wanawake,vijana na wakulima wadogo kushiriki katika kuongeza si tu uzalishaji lakini pia uongezaji wa thamani ya bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi.

Aidha imeshauri utoaji wa hamasa kwa wanawake wakulima ili washiriki katika uzalishaji wa mazao ya biashara yenye tija kipato kwa kutoa ruzuku maalumu za pembejeo, zana za kilimo, mitaji, elimu ya biashara na uhakika wa masoko kwa vikundi.

Mwisho kabisa TGNP imesisitiza kuwa rasilimali zilizotengwa za kuwezesha mchakato wa kupokea maoni ya wananchi kuhusu dira ya Taifa 2050, zitumike kuwafikia zaidi wananchi walioko katika maeneo yote hasa yaliyopembezoni na makundi maalumu hususan wanawake, watu wenye ulemavu, na vijana wa kike kwa wa kiume, na walioko katika sekta mbalimbali kwa misingi ya usawa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!