Kufuatia uwepo wa taarifa mbalimbali za matukio ya kutekwa na kuibwa kwa watoto katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Kanda ya Ziwa Victoria wametoa tamko la kuhusu hali ya usalama raia na wa watoto katika kanda hiyo.
Kupitia taarifa waliyoitoa juu ya matukio hayo, kanda ya Ziwa Mashariki inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu chini ya mratibu Sophia Donald, na Kanda ya Ziwa Magharibi inayojumuisha Mikoa ya Shinyanga, Geita na Kagera chini ya mratibu Madaga Joseph, wamerejea takwimu za hali ya uhalifu nchini Tanzania ya mwaka 2023 ambayo inaonesha kuwa kanda hiyo imekuwa na idadi kubwa ya ukatili kwa watoto.
“takwimu za Jeshi la Polisi mwaka 2023 jumla ya watoto 73 walitekwa ama kuibiwa na kati yao, watoto 33 walitekwa kutoka kanda ya ya ziwa. Lakini pia kwa kipindi cha mwaka 2005 hadi 2024 jumla ya matukio ya watu 20 ya mauaji au utekwaji wa watu wenye ualbino yamesharipotiwa kanda ya ziwa ambapo kwa mwaka wa 2024 ni matukio 3 yameshatokea na kuripotiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini.” Imeeleza THRDC-Kanda ya Ziwa.
Kupitia tamko hilo mtandao huo, umesema tamko lililotolewa na Rais Samia Suluhu mnamo Julai 20, 2024 alipozungumza na viongozi wa kimila mkoani Dodoma na kuwataka viongozi kuwajibika ipasavyo kudhibiti masuala hayo, izingatiwe na kuchukuliwa kwa uzito ili kukomesha matukio hayo.
“Sisi watetezi wa haki za binadamu tunaamini kwamba maelekezo ya Mhe. Rais si tu kwa viongozi wa serikali bali hata kwa viongozi wengine wa jamii kama viongozi wa dini pamoja na viongozi wa Mashirika yasiyo ya kutetea haki za binadamu. Hivyo, kutokana na msingi huo, sisi katika mkutano wetu mkuu wa kanda tumeweka mikakati mingi kuhusu kukabiliana na changamoto hii pamoja kuamua kutoa tamko hili kuhusu hali ya matukio ya utekwaji wa watu na watoto katika kanda ya ziwa.” Limeeleza tamko hilo.
Mbali na matukio mengine THRDC-Kanda ya ziwa imeyataja matukio matatu ya hivi karibuni yaliyotokea katika maeneo ya kanda ya ziwa, yaliyohusisha ukatili dhidi ya watoto wenye ualbino likiwamo tukio la mtoto Asiimwe Novathi (2) wa Muleba