Latest Posts

THRDC NA UMOJA WA ULAYA WATIA SAINI MAKUBALIANO YA KUIMARISHA UTAWALA BORA NA UWAJIBIKAJI

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umesaini mkataba wa Shilingi bilioni 4.1 (€1,500,000) kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kwa ajili ya kutekeleza mradi wa miaka minne kuanzia 2025 hadi 2028. Mradi huo, unaoitwa “Kulinda Utawala wa Sheria, Nafasi ya Asasi za Kiraia, na Uwajibikaji Tanzania kupitia Mashirikiano Yaliyoboreshwa,” unalenga kuimarisha utawala bora, nafasi ya kiraia, na uwajibikaji nchini Tanzania.

Katika utekelezaji wake, THRDC itashirikiana na mashirika matatu yenye uzoefu wa muda mrefu katika sekta ya sheria na haki za binadamu: Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS), Chama cha Wanasheria wa Afrika (PALU), na Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA).

Mradi huu unawalenga Asasi za Kiraia (CSOs), Vyama vya Wanasheria, na Taasisi za Serikali, ukilenga kuwawezesha kwa njia mbalimbali. Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kuimarisha uwezo wao wa kushawishi mabadiliko ya kisheria, kujenga mashirikiano ya kimkakati, na kutetea haki za jamii zenye mahitaji maalumu.

Shughuli mbalimbali zitatekelezwa kupitia mradi huu, ikiwa ni pamoja na mafunzo maalum kwa wadau wa haki za binadamu, usaidizi wa kiutendaji, na mazungumzo ya kimkakati yanayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, asasi za kiraia, na sekta nyingine muhimu za maendeleo. Lengo ni kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa, uwajibikaji unazingatiwa, na mageuzi endelevu yanatekelezwa kwa manufaa ya wananchi wote.

Utekelezaji wa mradi utaanza rasmi mwaka 2025, huku matarajio yakiwa ni kuleta mabadiliko chanya katika mfumo wa utawala na haki nchini Tanzania.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!