Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umelitaka Jeshi la Polisi Tanzania kumuachia mwandishi wa habari Bi. Dinna Maningo ambaye ameelezwa kushikiliwa na jeshi hilo tangu Juni 13, 2024.
Akizungumza na Jambo TV, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC Wakili Onesmo Olengurumwa amesema tuhuma alizokamatwa nazo si za msingi kwani alikuwa akitekeleza majukumu yake ya kitaaluma ambayo ni muhimu kwa ustawi wa jamii.
” Jeshi la Polisi wapaswa wamuone mwandishi huyo kama msaidizi wao kwa ajili ya taarifa nyingine nzuri za kiuchunguzi lakini tunasikitika mpaka leo (Juni 16, 2024) mwandishi huyu yupo ndani na tunataka mpaka kesho jioni (Juni 17, 2024) mwandishi huyu awe ameachiwa kwa dhamana kama kuna makosa ambayo anatuhumiwa nayo ili siku ya Jumanne aweze kufikishwa kwenye vyombo vya Mahakama twende tukamtetee” Ameeleza Wakili Olengurumwa.
Aidha Wakili Olengurumwa amesema kwamba wao kama THRDC wanasikitishwa na kufifishwa jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha mfumo wa haki jinai hautumiki kwa ajili ya kuumiza mtu
“Mtu hawezi kukamatwa bila uchunguzi kufanyika lakini pia suala la dhamana ni suala ambalo ni la haki ndiyo maana hata wakati wanazindua zile taarifa za Tume ya Haki Jinai tayari kuna sheria ya masuala ya dhamana inakwenda kutungwa, kwa hiyo tunakemea na tunataka hatua za haraka zichukuliwe kumuachia yule mwandishi vinginevyo tutachukua hatua za kisheria kwenda mahakamani kudai mwandishi yule aachiwe” Ameeleza Olengurumwa.
Taarifa kutoka kwa wakili wa Maningo zinaeleza kuwa mteja wake anakabiliwa na tuhuma za kuchapisha taarifa za siri za upelelezi ambazo bado hazijawekwa bayana.
Hata hivyo tovuti inayomilikiwa na Maningo ya Dimaonline imeelezwa na wafuatiliaji wa mambo kuwa ilikuwa ya kwanza kuchapisha habari kuhusu tuhuma za aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa simiyu za kumlawiti mwanachuo mmoja jijini Mwanza. RC huyo wa zamani naye yupo mikononi mwa polisi tangu Juni 11 2024
Taarifa zinaeleza kuwa Maningo, alikamatwa nyumbani kwake Tarime, mkoani Mara mnamo Juni 13, 2024 saa mbili usiku na kusafirishwa mpaka Mwanza ambako mpaka jioni ya Juni 15, 2024 Wakili wake amekuwa akishughulikia suala la kupata dhamana bila mafanikio huku kukiwa hakuna taarifa rasmi ya Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kuthibitisha kumshikilia mwandishi huyo wa habari.