Latest Posts

THRDC YAZINDUA KAMATI YA UHAMASISHAJI UPATIKANAJI WA RASILIMALI ZA NDANI

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umetangaza kamati yake iliyoanzishwa kwa lengo la kuhamasisha upatikanaji wa rasimali za ndani ili kuimarisha utetezi na ulinzi wa haki za binadamu Tanzania kwa kutumia njia mbalimbali za kutafuta fedha.

Akizungumza mbele ya vyombo vya habari Jumatatu Juni 10, 2024 Mratibu Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa amesema kuwa kamati hiyo imeundwa na wakurugenzi 26 wa taasisi zinazotetea haki za binadamu ili kufanikisha lengo hilo.

Wakili Olengurumwa amesema kuwa THRDC inathamini kazi ya ukuzaji na ulinzi wa haki za binadamu inayofanywa na watendaji mbalimbali japo mashirika mengi ya kutetea haki za binadamu yanakabiliwa na uhaba wa kiufundi na kifedha  hivyo wengi wao hufanya kazi kwa hiari bila kupata rasilimali fedha kutoka kwa wafadhili wa ndani au washirika wa nje.

Akielezea malengo ya kamati hiyo Wakili Olengurumwa amesema kuwa kamati inalenga kufanya kazi kwa karibu na wafanyabiashara na kampuni ili kuunganisha mikakati ya Uwajibikaji kwa Jamii (Corporate Social Responsibility) ambayo inalingana na mipango ya haki za binadamu ili ushirikiano huo uweze kuwa na athari chanya za uwajibikaji kwa jamii na kushughulikia changamoto kuu za haki za binadamu katika jamii.

Kwa upande wake Lissa Filbert mkuu wa Idara ya wanachama THRDC amezikaribisha jumuiya za sekta binafsi nchini kuunga mkono hatua hiyo akisema kuwa faida za kusaidia shughuli za haki za binadamu ni nyingi ikiwamo ushirikishwaji wa jamii kuongezeka na kuongezeka kwa matokeo chanya kwa jamii kupitia juhudi za wahisani.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!