Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umezindua Mtandao wa watoto wanaotetea haki za binadamu (Tanzania Child Rights Forum) kwa lengo la kuwajengea watoto uwezo wa kusimamia haki zao wenyewe na wengine katika jamii yao.
Uzinduzi huo umefanyika Ijumaa Juni 14, 2024 katika maadhimisho kuelekea siku ya mtoto wa Afrika tarehe 16 Juni yaliondaliwa na THRDC ikishirikiana  na wadau wengine watetezi wa haki za binadamu ambao ni Save The Children, TCRF, Bright Hope school na East African Human Rights Institute, yaliyofanyika shule ya sekondari Alpha iliyopo Mikocheni B, jijini Dar es Salaam mbapo watoto kutoka shule za jiji hilo za Bright Hope, Jerusalem na Alpha high school wameshiriki.
Akizungumzia uzinduzi huo Mratibu Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa amesema kuwa watoto wengi wanafanyiwa ukatili kutokana na kutokujua haki zao na namna ya kujitetetea hivyo mtandao huo utakuwa na msaada kwao.
“Ukatili ni mkubwa sana kwa watoto majumbani, shuleni na mtaani, na hii inachangia kuvunja haki za watoto kwani unakuta hata ile nafasi ya kujitetea haipo. Mtoto akiwa amefundishwa kujitetea ni rahisi sana kutetea haki zake.” Amesema Olengurumwa.
Kwa upande wake mkuu wa shule ya sekondari Alpha, Fulgence Kabiligi amesema kuwa shule yao inaunga mkono jitihada zinazofanywa na THRDC katika kuhakikisha haki za binadamu zinasimamiwa na makundi yote.
Pia katika uzinduzi huo watoto wamechagua viongozi ambao watakuwa wasimamizi wa makundi hayo ambapo Naomi Ombeni kutoka shule ya sekondari Alpha amechaguliwa kuwa Rais wa mtandao huo.