Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri amesema kituo hicho kimekusanya na kusajili miradi zaidi ya 240 katika mkoa wa Iringa, yenye mitaji ya dola bilioni 8 (Shilingi za Kitanzania trilioni 21.68) na yenye uwezo wa kutoa ajira kwa zaidi ya watu 28,000.
Â
Teri ameyasema hayo alipofanya mkutano na wawekezaji mkoani Iringa tarehe 22 Agosti 2024 ambapo amesisitiza umuhimu wa Iringa kama mkoa wa kimkakati kwa uwekezaji ukitoa fursa za uwekezaji katika sekta za kilimo, viwanda, uchukuzi, na utalii.
Â
Amesema kuwa sekta ya kilimo inatoa nafasi za kupanua uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao, sekta ya viwanda ikitoa mwanya wa kuanzisha viwanda vya kubadilisha malighafi kuwa bidhaa zenye thamani zaidi, uchukuzi ukitoa fursa za kuboresha miundombinu, na utalii ukitoa nafasi za kukuza maeneo yenye vivutio vya kipekee kama vile Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo sasa inachukuliwa kuwa Serengeti mpya kutokana na ongezeko la watalii.
Â
Aidha Teri amegusia pia athari za Royal Tour katika kukuza sekta ya utalii nchini akieleza kuwa mpango huo umeleta ongezeko kubwa la idadi ya watalii wanaotembelea maeneo mbalimbali ikiwamo Ruaha kutokana na kubainisha vivutio vya kitalii vya Tanzania na kuvifanya kuwa maarufu zaidi duniani.
Â
Halikadhalika Teri amehimiza ushirikiano wa karibu kati ya TIC, wawekezaji, na viongozi wa mkoa ili kuhakikisha kuwa fursa hizo zinaweza kutumika kikamilifu na changamoto zinatatuliwa kwa ufanisi.
Â
Mkutano huo ambao ulihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Kheri James, ulilenga kuwapongeza wawekezaji kwa juhudi zao, kuwajuza kuhusu fursa zinazopatikana, na kusikiliza changamoto wanazokumbana nazo katika shughuli zao za uwekezaji, huku ukiwa jukwaa muhimu kwa mazungumzo yaliyolenga kuimarisha mazingira ya biashara na kuongeza uwekezaji katika mkoa wa Iringa.