Meneja wa Kanda ya Kati Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Venance Mashiba amesema kwa mwaka 2024, mkoa wa Dodoma umefanikiwa kusajili miradi 46 ya wawekezaji wa ndani na nje jambo ambalo halijawahi kutokea huko nyuma hapo awali.
“Mwaka huu 2025, Kuanzia Mwezi Januari hadi Mwezi Mei tumesajili miradi ipatayo 14, tunaweza kujivunia kwamba kituo kinapiga hatua kubwa katika kuhamasisha na kuhudumia wawekezaji” alisema Mashiba.
Bw. Mashiba ameyasema hayo Juni 18,2025 alipokuwa akizungumza na Waandishi Wa Habari katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dooma kwenye Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza Juni 16,2025 na kutarajiwa kuhitimishwa Juni 23,2025.
Kwa upande mwingine, Meneja Mashiba amesema mbali na kuvunja rekodi ya usajili kwa mwaka 2024, Kituo hicho kimepanga kuongeza usajili wa miradi mpaka kufikia 1,500 kwa mwaka 2025.
Aidha, Meneja Mashiba ametoa wito kwa wadau na wakazi wa jiji la Dodoma kujitokeza kwa wingi kwenye maonesho hayo ili waweze kujifunza mambo mbalimbali juu ya kituo hicho cha uwekezaji TIC.