Latest Posts

TIC YAWAHAMASISHA WAFANYABIASHARA KARIAKOO KUANZISHA VIWANDA BADALA YA KUAGIZA BIDHAA

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeanza mpango maalum wa kuwahamasisha wafanyabiashara wa soko la Kariakoo kuacha kuishia katika biashara ya uuzaji wa bidhaa kutoka nje na badala yake waanze kuwekeza katika viwanda vya uzalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini.

Akizungumza siku ya Ijumaa Mei 16, 2025 katika ziara ya TIC kwenye soko hilo maarufu jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Gilead Teri amesema lengo la mpango huo ni kuwabadilisha wafanyabiashara kutoka kwenye mfumo wa uagizaji bidhaa na kuwa wawekezaji wanaozalisha bidhaa hizo hapa nchini, kwa kutumia soko walilonalo tayari.

 

“Watanzania wengi wamezoea kufanya biashara kwa kununua bidhaa nje ya nchi na kisha kuziuza hapa nyumbani. Sisi tumekuja kuwashawishi kuwekeza hapa nchini. Wana soko, wana wateja, sasa waanze kuzalisha bidhaa hizo hapa nchini,” amesema Teri.

Amesema TIC imekutana na zaidi ya wafanyabiashara 100 katika zoezi hilo la kwanza, ambalo ni endelevu na litafanyika kila mwezi kupitia kanda ya Mashariki. Aidha, ametaja maeneo matano yenye fursa kubwa ya uwekezaji kuwa ni bidhaa za ujenzi, vifaa vya nyumbani, nguo na bidhaa za pamba, usindikaji wa mazao ya kilimo na bidhaa za mbao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kariakoo, Severin Mushi, ameunga mkono mpango wa TIC na kusema kuwa hatua hiyo itawawezesha kuvuka hatua moja kwenda nyingine. Hata hivyo, ameiomba TIC kuangalia uwezekano wa kupunguza kiwango cha ada ya usajili ili iwavutie wafanyabiashara wengi zaidi kuwekeza.

Severin Mushi

Naye mfanyabiashara wa Kariakoo, Johnson Minja, ameiomba TIC kuanzisha utaratibu wa kutambua wafanyabiashara wa eneo hilo na aina ya biashara wanazozifanya, kwa lengo la kuwashirikisha moja kwa moja katika miradi ya pamoja ya uwekezaji, kwa kuunganishwa na wawekezaji wanaokuja nchini. Amependekeza kuwa iwapo hatua hiyo itafanikiwa, basi Watanzania wafaidike zaidi kwa kupewa kipaumbele.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!