Latest Posts

TLS: MASHTAKA YA LISSU NI TISHIO KWA SHERIA NA DEMOKRASIA

Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society – TLS) kimetoa taarifa ya kulaani kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha DEmokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Antipas Lissu, kikieleza kuwa tukio hilo ni kinyume na misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haki za binadamu na utawala wa sheria.

Akizungumza katika taarifa ya tarehe 11 Aprili 2025 kwa niaba ya Baraza la Uongozi la TLS, Rais wa chama hicho, Wakili Boniface Mwabukusi, amesema: “Kukamatwa na kushikiliwa kwa Wakili Tundu Lissu si tu kinyume na sheria, bali pia ni tishio la moja kwa moja kwa heshima ya taaluma ya sheria, haki za kikatiba na mustakabali wa demokrasia nchini.”

TLS imeeleza kusikitishwa na mazingira ya ukamataji, ikibainisha kuwa yalikiuka haki mbalimbali zikiwemo uhuru wa kutoa maoni, haki ya kujiunga na vikundi, na taratibu za msingi za mwenendo wa mashauri ya jinai.

TLS imetaja ukiukwaji wa wazi wa Katiba na Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai katika tukio hilo, ukiwemo kukamatwa bila hati halali, kunyimwa mawasiliano na wakili wake au familia, matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wa ukamataji na kukosekana kwa maelezo ya kosa analotuhumiwa nalo

Kwa mujibu wa TLS, hali hiyo inakiuka masharti ya Vifungu vya 11, 12, 14, 21, 23 na 54 vya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura ya 20. Katika taarifa yake, TLS imeeleza wasiwasi mkubwa juu ya mashtaka ya uasi dhidi ya Lissu, ikisema: “Uongozi wa kisiasa hauwezi kuchukuliwa kama kitendo cha uasi bila ushahidi wa wazi na wa kisheria. DPP anapaswa kuwa makini katika matumizi ya mashtaka mazito kama haya.”

TLS pia imeonya kuwa matumizi ya vyombo vya dola dhidi ya wanasiasa yanaweza kuchochea taharuki ya kitaifa.

Baraza la Uongozi la TLS limetoa mapendekezo tisa, likiwemo kuachiwa huru kwa Lissu mara moja bila masharti, kufanyika kwa mageuzi ya kisiasa na kisheria ili kulinda usawa na haki, kuweka mbele mazungumzo ya kisiasa kati ya vyama na kuimarishwa kwa weledi wa kisheria katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Mamlaka za Mashtaka

TLS pia imetishia kusitisha huduma za uwakilishi wa dock brief na huduma nyingine za kujitolea, iwapo vitendo vya unyanyasaji wa kisheria vitaendelea.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!