Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimelaani kukamatwa kwa viongozi wa kisiasa hususani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mawakili, waandishi wa habari waliokuwa wakitekeleza majukumu yao na wanaharakati mbalimbali kulikofanywa na Jeshi la Polisi katika mkoa wa Iringa na Mbeya.
Kupitia taarifa iliyotolewa Jumatatu Agosti 12, 2024 na Baraza la Uongozi la chama hicho chini ya Rais wake Boniface Mwabukusi, TLS imebaini kuwepo kwa kamatakamata iliyo kinyume cha sheria kwa siku za karibuni ikieleza kuwa ina lengo la kuyanyima makundi hayo haki yao ya msingi na ya kikatiba ya uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kujumuika huku ikilinyooshea jeshi la polisi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kile ilichokieleza kuwa ubaguzi na upendeleo kwa upande mmoja.
“Jeshi la Polisi pamoja na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa imekuwa na uzito mkubwa katika kuchukua hatua za kisheria kwa wahusika hasa pale zinapotolewa kauli zenye viashiria vya uhalifu kutoka kwa upande wa viongozi wa Chama Tawala”, imeeleza TLS.
TLS imeelezwa kusikitishwa na ukamataji uliotokea ikiueleza kufifisha uhalisia wa 4R za Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambazo ni maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya ambazo Rais amekuwa akizihubiri tangu alipoingia madarakani.
Aidha TLS imetoa wito na kulisihi Jeshi la Polisi nchini kuheshimu utawala wa sheria na mara zote lijielekeze katika kulinda raia na mali zao, na kuacha kuingilia shughuli za vyama vya siasa na za makundi mengine, badala yake liimarishe uwezo wake wa kuvilinda wakati vinapotaka kutumia haki zao za kikatiba katika shughuli zao kwa mujibu wa taratibu na sheria.
TLS imesema kuwa imepitia maelezo ya Jeshi la Polisi na ya kile kinacholalamikiwa kuwa kauli yenye kuhatarisha usalama, na kufikia hitimisho kwamba hakukuwa na sababu yoyote ya polisi kutumia nguvu kubwa kama ilivyofanya kwani kauli zile zilikuwa za kiujumla na za kisiasa zisizokuwa na viashiria au uthibitisho wa uhalifu ndani yake.
TLS kupitia kamati maalumu ya mawakili imeelekeza kufanyike tathmini na kuchukuliwa kwa hatua stahiki za kisheria kwa kila afisa aliyehusika kusababisha “kadhia hii” kwa jina lake na kuhakikisha utii na uzingatiwaji wa matumizi bora ya madaraka katika Ofisi za Umma.
TLS pia imetoa wito kwa viongozi wengine wa nchi na wa kisiasa kuacha mara moja kutoa matamko au matamshi ambayo yanaweza kuleta taharuki katika jamii na kuchochea hasira au malalamiko kutoka makundi mengine ya jamii, na kutoa wito pia kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufanya kazi yake kwa mujibu wa Katiba na Sheria bila upendeleo wowote.