Latest Posts

TLS YASIKITISHWA NA ONGEZEKO LA MAUAJI NA UTEKAJI KINYUME NA KATIBA

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimeonesha kusikitishwa kwake na kuendelea kushamiri kwa matukio ya utekaji na mauaji ya kikatili nchini, yakiwemo yale ya hivi karibuni yaliyohusisha kutekwa na kuuawa kwa mwanasiasa na kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ali Mohamed Kibao.

Katika tamko lao la tarehe 10 Septemba 2024 lililotolewa na Baraza la Uongozi la TLS chini ya Rais wake Boniface Mwabukusi, chama hicho kimeeleza kuwa matukio haya yamekiuka haki za msingi za kikatiba, hususan haki ya kuishi, haki ambayo imeainishwa kwenye Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa TLS, tukio la kuuawa kwa Ali Mohamed Kibao lilipokelewa kwa huzuni kubwa, huku taifa likiwa bado halijasahau tukio jingine la kikatili lililotokea tarehe 6 Septemba 2024, ambapo mwanamke aliyejulikana kwa jina la Mwamvita Mwakibasa na mtoto aliyejulikana kama Salma Ramadhan, walikutwa wameuawa kinyama katika eneo la Kata ya Mkonze, jijini Dodoma.

TLS limeeleza kuwa matukio haya yameleta wasiwasi mkubwa kwa wananchi kuhusu hali ya usalama wao na mustakabali wa haki zao za kikatiba.

“TLS inapenda kuvikumbusha vyombo vya dola juu ya majukumu yake ya kikatiba na kisheria ya kulinda watu na mali zao. Haki ya kuishi na kulindwa kwa kila mwananchi ni haki iliyoelezwa kwenye Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, kumekuwa na ongezeko la watu kutekwa na hatimaye kupatikana wameuawa, kitu ambacho ni kinyume na Katiba ya nchi yetu,” ilisema sehemu ya tamko hilo.

Katika tamko hilo, TLS imetoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuunda tume maalum huru itakayochunguza matukio haya ya uhalifu ili kupata suluhu ya kudumu na kurejesha imani ya wananchi katika haki zao za msingi na uhuru wao.

TLS imeeleza kuwa ni muhimu kwa serikali kuhakikisha kuwa matukio haya yanashughulikiwa kwa kina na kwa uwazi ili kuleta matumaini kwa wananchi kuwa haki itatendeka.

Aidha, TLS imetoa wito kwa vyombo vya usalama, hususan Jeshi la Polisi, kuhakikisha vinatoa maelezo sahihi kwa umma kuhusu watu waliotekwa kinyume cha sheria na kueleza hatua ambazo tayari zimechukuliwa kuhakikisha watu hao wanapatikana. TLS imesisitiza kuwa ni muhimu kwa vyombo vya dola kufuata taratibu na sheria wakati wa ukamataji wowote ili kuepuka ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Jeshi la Polisi lihakikishe kwamba linatoa taarifa sahihi kwa umma dhidi ya watu wote waliochukuliwa na kutekwa kinyume na sheria kwa kueleza taratibu walizochukua mpaka sasa kwa lengo la kuhakikisha watu hao wanapatikana,” ilisisitiza TLS katika tamko lake, likiongeza kuwa ni muhimu kwa kila ukamataji kufanywa kwa kushirikisha viongozi wa serikali za mitaa husika ili kudumisha uwazi na haki.

Katika jitihada za kuhakikisha kuwa haki inatendeka, TLS limependekeza kuvunjwa kwa vikosi kazi vyote vilivyoundwa kinyume cha sheria na ambavyo vimekuwa vikifanya kazi nje ya misingi ya sheria. TLS limeeleza kuwa vikosi hivi vinachangia katika kuvuruga utawala wa sheria na amani ya wananchi.

“IGP atoe tamko la kuvunjwa kwa vikosi kazi vyote vilivyoundwa ambavyo vimekuwa vikifanya kazi kinyume na sheria za nchi na kuelekeza kwamba ukamataji wowote kabla ya kufanyika lazima awepo kiongozi wa Serikali ya Mtaa husika,” ilisema TLS, ikionesha wasiwasi wake juu ya vikosi vinavyofanya kazi bila kuzingatia taratibu na sheria za nchi.

Kwa kuzingatia hali hii, TLS imeeleza kuwa imeanza kupitia baadhi ya sheria zilizopitishwa na Bunge ambazo zinaonekana kutoa mianya kwa vikundi fulani kufanya kazi zao bila kuzingatia misingi ya haki. TLS imeahidi kuzifikisha sheria hizi mahakamani na kuzipinga kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Aidha TLS imetoa pole kwa familia ya Ali Mohamed Kibao, Mwamvita Mwakibasa, na Salma Ramadhan kwa vifo vya wapendwa wao, huku ikieleza kusikitishwa kwake na matukio haya ya kikatili. TLS pia imetoa pole kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kupoteza mwanachama wao, Ali Mohamed Kibao.

TLS imehitimisha tamko lake kwa kutoa wito kwa serikali na vyombo vya usalama kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa wahanga wa matukio haya ya uhalifu, na kusisitiza kuwa vyombo vya dola vina jukumu la kikatiba la kulinda raia na mali zao, kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!