Latest Posts

TPA MWAJIRI BORA SEKTA YA UMMA 2024

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa mara ya tatu mfululizo imetangazwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kuwa ni Mwajiri Bora wa Sekta ya Umma 2024, na kupewa Tuzo ya Mwanachama wa Kudumu kwa Taasisi za Umma.

Akiukabidhi uongozi wa TPA tuzo za umahiri mwishoni mwa juma, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, akimwakilisha Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, amewapongeza wafanyakazi na viongozi wa TPA kwa ushindi wa tuzo hizo, na kuitaka mamlaka kuendeleza juhudi ambazo zimeifanya ishinde tuzo mara tatu mfululizo.

Dkt. Biteko amekumbusha kwamba TPA ni taasisi ya kitaifa ya kiuchumi na ya kimkakati na kueleza furaha yake kwa utendaji wa TPA ambao umetambuliwa na ATE pasipo upendeleo wowote.  Amesema TPA siyo tu inafanya vizuri kiuchumi bali imeonesha kwamba ni mwajiri wa kupigiwa mfano nchini.

Dkt. Biteko alitumia fursa hiyo kuwafikishia wafanyakazi na uongozi wa TPA salamu za Makamu wa Rais Dkt. Mpango ambaye aliwatakia mafanikio zaidi katika siku zijazo.

Akiwa katika hafla hiyo, Naibu Waziri Mkuu alielezwa kwamba TPA haikushinda tu Mwajiri Bora wa Sekta ya Umma, bali pia imetwaa tuzo nyingine nne ikiwemo kuongoza kwenye Tuzo ya Mwajiri Bora Mzawa (Local Employer Award), kutangazwa kuwa mshindi wa pili wa jumla kwa sekta zote kwa kupewa tuzo ya 2nd Runners-Up.

Aidha TPA ilitambuliwa kama moja ya taasisi zinazofanya vizuri sana na kupewa Tuzo ya Club of Best Performers, na kupongezwa kwa uanachama wa muda mrefu wa ATE na kupewa Tuzo ya Mwanachama wa Kudumu kwa Taasisi za Umma.

Dkt. Biteko alifahamishwa kuwa tuzo hizi hutolewa kila mwaka na ATE kwa waajiri kutoka sekta za umma na binafsi ambao wameonesha utendaji bora na ubunifu katika mwaka husika. Imeelezwa kuwa ushindi wa TPA ni uthibitisho wa dhamira yake ya kuboresha ustawi wa wafanyakazi, kuboresha mazingira ya kazi na kuendelea kuchangia maendeleo ya sekta ya bandari nchini.

Mwaka huu TPA ilitoa kwa serikali gawio la Shilingi bilioni 153.9 na kuwa taasisi iliyotoa gawio la juu kabisa.  Kampuni 145 zilikabidhi kwa Rais Samia Suluhu Hassan jumla ya Shilingi bilioni 636 ikiwa ni gawio kwa serikali, ambapo taasisi za kibiashara zilitoa bilioni 278 na mamlaka za udhibiti zilitoa bilioni 358.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!