Wataalam wa Mipangomiji na Kampuni za Upangaji Miji nchini Tanzania amabao wana sifa na bado hawajasajiliwa wametakiwa kutuma maombi ya usajili ili waweze kusajiliwa rasmi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji (TPRB), TP. Martha Mkupasi siku ya Jumatatu jijini Dodoma wakati akieleza hali ya usajili wa wataalam pamoja na kampuni za upangaji miji nchini.
Amesema kuwa mpaka kufikia Mei 2025 Bodi hiyo imeweza kusajili wataalamu 514 wa mipango miji huku ikisajili kampuni 99 zanazotoa huduma za mipango miji, hivyo wataalamu wote ambao wana sifa lakini bado hawajasajiliwa nchini wanapaswa kujisajili.
Amesema kuwa Bodi hiyo inapokea maombi ya watalamu hao kwa ajili ya usajili, akieleza kuwa maombi hayo yawasilishwe katika Ofisi ya Msajili kabla ya Septemba 23, 2025, ambapo Bodi hiyo inatarajia kufanya kikao cha kusajili wataalamu hao na kampuni za upangaji miji mwishoni mwa mwezi Septemba.
“Napenda kuwataarifu watalaam wa Mipangomiji wote wenye sifa ya kusajiliwa na ambao bado hawajasajiliwa kuwa Bodi inategemea kufanya kikao cha kusajili watalaam wa Mipamgomiji na Kampuni za Upangaji Miji mwishoni mwa mwezi Septemba, hivyo wale wote wenye sifa pampoja na makampuni yanayohitaji kutoa huduma za mipango miji watume maombi kabla ya muda huo haujaisha ili tuweze kupitia na kuwapa usajili” ameeleza TP Mkupasi na kuongeza;
“Tunaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali itakayowawezesha wataalamu wenye sifa kutokufanya kazi hizo bila kusajiliwa na ni kinyume na sheria kufanya kazi hizo bila usajili” amesisitiza
TP. Mkupasi amesema kuwa Bodi hiyo itaendelea kusimamia maadili na nidhamu ya utendaji kazi kwa wataalam wa mipangomiji, kutoa ushauri wa kitaalam Pamoja na kuchunguza ukiukwaji wa maadili utakaofanywa na wataalam wa mipangomiji na makampuni ya mipango miji