Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa itawachukulia hatua wafanyabiashara wenye asili ya China ambao baadhi yao wanaenda kinyume na sheria za kodi kwa kukwepa kulipa kodi.
Akizungumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo kuhusu changamoto zinazowakabili, Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda amebainisha kuwa TRA hupokea taarifa kuhusiana na yeyote anayekwepa kodi na hufuatilia, na ikithibitisha huchukua hatua kwa mujibu wa sheria za kodi.
Katika hatua nyingine Mwenda amesema wamekubaliana na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo kuunda kamati ya pamoja ambayo itahusisha watumishi wa Kariakoo mkoa wa kikodi wa Kariakoo pamoja na wafanyabiashara ambayo itakuwa inakutana kila wiki mara moja yaani mara nne kwa mwezi.
Kamati hiyo itabaini na kutatua changamoto mbalimbali kwa haraka ikiwamo matatizo ya kikodi na changamoto zilizopo ambazo zinazuia kuifanya Kariakoo kuwa soko la kimataifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo Martin Mbwana amesema wamezungumza mambo mengi kwa masilahi mapana ya maendeleo ya Kariakoo na nchi kwa ujumla ambayo yamepelekea Kamishna Mkuu wa TRA kukubali na kuridhia uhusiano wa karibu kati ya TRA na wafanyabiashara wa Kariakoo kwa kuunda kamati ya pamoja itakayojumuisha pande hizo mbili.