Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Mtwara imetoa msaada wenye thamani ya Shilingi milioni 12 kwenye vituo vya kulelea watoto yatima na wale waishio kwenye mazingira magumu.
Akizungumza Machi 28, 2025 baada ya kukabidhi misaada hiyo, Meneja wa TRA mkoani humo Maimuna Khatibu amesema wametoa msaada huo kwenye vituo viwili vilivyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani, Masasi na Newala ili uweze kuwasaidia watoto hao katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani pamoja na Sikukuu ya Eid El- Fitr.
Katibu wa Baraza Kuu la Wanawake wa Kiislamu Tanzania mkoa wa Mtwara, Aisha Suleiman amesema wao kama wanawake wanazijua changamoto kubwa ambazo watoto ambao hawana wazazi wanakutana nazo hali iliyosababisha kuanzisha kituo hicho cha watoto ili waweze kuwapa faraja ingawa majukumu ya kulea watoto hao ni makubwa tofauti na kipato cha walezi hao.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Morovian Usharika wa Mtwara, Kenedy Kalago amewashukuru TRA kwa kufuata maandiko ya kitabu cha Biblia ambayo yanasema dini iliyo nzuri ni ile inayowajali yatima, wajane na wanaoishi kwenye mazingira magumu, na kuongeza kuwa kupitia msaada huo utasaidia kuwahamasisha wanafunzi kusoma kwa bidii ili na wao waje kusaidia wenzao wenye uhitaji.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Mtwara Mikindani, Swaumu Omary amesema idadi ya watoto wenye uhitaji ni kubwa ukilinganisha na wadau wanaojitolea kuwasaidia lakini pia wapo baadhi ya wazazi hawaguswi kuwapeleka watoto shule. Hivyo ametoa rai kwa jamii kutoa taarifa kwenye ofisi za kata ili waweze kuwasaidia watoto hao waweze kutimiza ndoto zao.